WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Doroth Gwajima, ameendelea 'kumkalia kooni' Askofu Joseph Gwajima kwa kumtaka athibitishe madai yake ya kiongozi wa serikali kuhongwa ili kuruhusu chanjo ya UVIKO-19 nchini.
Amesema amekamilisha taratibu zote za kisheria ikiwamo kuandika barua rasmi kwa vyombo vya usalama ili vianze kumhoji Askofu Gwajima.
Juzi Dk. Dorothy aliomba vyombo vya usalama kumhoji Askofu Gwajima, lakini Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, alisema jeshi hilo haliwezi kufanya kazi hiyo bila kupata barua rasmi kutoka katika mamlaka husika.
Akizungumzia kauli hiyo ya IGP Sirro, Dk. Dorothy alisema kiongozi huyo wa Jeshi la Polisi yupo sahihi kwa kuwa vyombo vya usalama haviwezi kuanza kumhoji mtu bila kupata malalamiko rasmi kutoka kwa mlalamikaji ambaye ni yeye.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya kuzungumza na watumishi wa Sekta ya Afya pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali jijini Mwanza, waziri huyo alisema hakuagiza Askofu Gwajima akamatwe bali alitaka aitwe na kuhojiwa.
"Juzi nikiwa Butiama niliagiza vyombo vya usalama kumhoji Askofu Gwajima ili athibitishe madai yake kwamba viongozi wa serikali wamehongwa ili kuruhusu kuingiza chanjo ya UVIKO-19,'' alisema.
Alisema anataka Askofu Gwajima aitwe na kuhojiwa ili aeleze nani kahongwa, lini alihongwa, wapi alipewa fedha hizo na zilikuwa kiasi gani.
Kuhusu upotoshaji wa chanjo ya UVIKO-19, waziri huyo alisema kuna watu wengi wanapotosha suala hilo na kwamba kila mtu mwenye simu, atafute habari zake na kuzisoma ili afanye uamuzi badala ya kusikiliza mambo ya watu.
Dk. Dorothy alisema mtu akichanjwa ni rahisi mwili wake kupambana na ugonjwa wa corona kama ukimpata kuliko yule ambaye hajachanja.
“Wengi hawakusikiliza kipindi cha awamu ya tano, ndiyo maana wanauliza mbona mlisema hivi, Hayati Rais John Magufuli katika hotuba yake alisema msiwe mnakimbilia chanjo hadi mjiridhishe, hakusema msichanje," alisema.
Waziri huyo alisema kuna watu wanatembea na kivuli cha Hayati Rais Magufuli kwa kuwa na ajenda zao zinazopotosha.
Akizungumzia tiba asili, alisema chanjo haifuti tiba hizo na kuwapiga marufuku watu wanaogeuza Wizara ya Afya kuwa ajenda ya kisiasa.
Kuhusu takwimu za vifo vilivyotokana na ugonjwa wa corona, Dk. Dorothy alisema bado zinaandaliwa na muda siyo mrefu zitatolewa kwa nchi nzima.
"Hizi takwimu tunazo, zikiwa tayari zitatolewa kwa nchi nzima kwa sababu zipo wazi na kila mtu ataziona na kuzisoma,'' alisema.
Katika hatua nyingine, waziri huyo alizungumzia ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Mwanza (Sekou Toure), akisema serikali imepitisha bajeti ya Sh. bilioni sita kwa mwaka wa fedha 2021/22 kwa ajili ya kumalizia jengo hilo.
Aliagiza kufikia Desemba mwaka huu jengo hilo liwe limekamilika na kuanza kutoa huduma kwa mama wajawazito.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel akizungumza hospitalini hapo, alisema jengo hilo lipo katika hatua nzuri na kumwomba Dk. Gwajima kuwaongezea fedha kwa ajili ya kukamilisha ili kufikia Desemba lianze kutoa huduma.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa jengo hilo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Bahati Peter, alisema ujenzi huo ulianza Oktoba 2017 chini ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na gharama za mradi ni Sh. bilioni 10.1 na kwamba fedha zilizopokewa hadi sasa ni Sh. bilioni 9.8.
Meneja wa Wakala wa Majengo (TBA) Mkoa wa Mwanza, Bernad Mayemba, alisema ujenzi huo umefanyika kwa mfumo wa ujenzi na usimamizi kwa kufuata mchoro na kuzingatia ubora wa vifaa vilivyotumika.