Rais wa Marekani Joe Biden ametetea uamuzi wake wa kuondoa majeshi yake nchini Afghanistan licha ya nchi hiyo kutekwa na Taliban haraka mno.
Hata hivyo, Biden amekubali kuwa matokeo yaliyochangia Taliban kupindua serikali ya Afghan na kuchukua madaraka yalitendeka kwa "haraka sana kuliko ilivyotarajiwa".
"Wamarekani hawawezi na hawastahili kupigana vita au kufariki dunia katika vita ambavyo Waafghan wenyewe hawako tayari kujipigania," Biden amesema kutoka Ikulu ya Marekani.
"Nasalia kuwa thabiti na uamuzi wangu," ametoa hakikisho.
Jumapili, Taliban walitangaza ushindi baada ya rais wa Afghan Ashraf Ghani kutoroka nchi na serikali yake ikaporomoka.
Wanamgambo wenye msimamo mkali wanarejea serikalini baada ya karibu miaka 20 ya uwepo wa muuungano ulioongozwa na Marekani ambao umeshindwa.
Biden anakabiliwa na ukosoaji mkubwa kisiasa kutokana na uamuzi wake wa Aprili kuagiza wanajeshi wote wa Marekani kuondoka Afghanistan kufikia Septemba 11, maadhimisho ya miaka 20 tangu kutokea kwa shambulizi lililochochea Marekani kuvamia nchi hiyo.
Rais alisema kuwa lengo la miaka 20 halikuwa "kujenga nchi," bali kuzuia mashambulizi ya kigaidi katika ardhi ya Marekani.
"Sitapitisha jukumu hili kwa rais wa tano," ameelezea, akirejelea jambo ambalo amekuwa akilisema tangu alipofanya uamuzi wake wa kuondoka Afghanistan mnamo mwezi Septemba.
"Nimesikitishwa sana na matukio tunayokabiliana nayo sasa hivi lakini sijutiii uamuzi wangu wa kumaliza vita vya Marekani nchini Afghanistan.