Dodoma. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima amepewa pole na kutakiwa awe mvumilivu kama Yesu.
"Kumbuka hata Yesu hakukubaliwa kwao, walimdhihaki na kumzodoa lakini wakamweka msalabani kwa ajili ya watu wake," amesema Stanslaus Nyongo ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii.
Nyongo ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Agosti 26, 2021 wakati akizungumza kwenye ziara ya kamati hiyo katika kituo cha kulea watoto cha Kikombo.
Hata hivyo, hakufafanua zaidi kauli yake hiyo ilikuwa inalenga nini.
Siku za hivi karibuni Dk Gwajima ameingia kwenye mtafaruku na mbunge wa Kawe (CCM), Askofu Josephat Gwajima kuhusu chanjo wa Uviko-19.
Nyongo amesema kazi zinazofanywa na waziri huyo ni kwa faida ya Watanzania sio za kwake binafsi, hivyo asiogope wala kuhofia anaporushiwa maneno makali na watu wengine.
Akizungumza kuhusu chanjo, Nyongo amedai kinachosumbua wakati wote ni elimu kwa watu kwani hawajakataa kuchanja ila wanahoji kwa ajili ya kupata uelewa.