Kauli ya Baba Mzazi wa Haji Manara Baada ya Kutua Yanga "Wametekeleza Aliyosema Jakaya Kikwete"




YANGA ni kama wametekeleza rai iliyowahi kutolewa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alipowaambia viongozi na wanachama wa Yanga, wasilalamike juu ya mchezaji Bernard Morrison alipotua Simba na kuwataka na wao watafute wa kumchukua yeyote wanayemuona anawafaa.

Juzi jioni Yanga ilimtambulisha aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, huku ikizua mjadala, lakini baba yake mzazi, Sunday Manara amesema mwanaye kujiunga na Yanga hajakosea kwani ni matakwa yake kwa maana ya kwamba hakuna ushawishi aliompa.

Nyota huyo wa zamani wa kimataifa, aliyekuwa Mtanzania wa kwanza kucheza soka la kulipwa Ulaya na aliyewahi kuwa katika kamati mbalimbali za klabu hiyo, alisema haoni tatizo kwa mwanae kutua Yanga.

Manara aliachana na Simba baada ya mkataba wake kumalizika huku akiondoka Msimbazi akilalamikiwa kuihujumu timu hiyo, na juzi kwenye utambulisho wake alisema alikubali kujiunga Yanga kutokana na dau walilotoa kwani alikuwa na ofa zaidi ya hiyo mezani kwake, hivyo ameenda kufanya kazi.


“Sitaki kuzungumzia ishu za Haji na Simba na Yanga kiundani, kwa kuwa kote alikopita ni uamuzi wake binafsi katika utendaji kazi,” alisema Mzee Sunday.

Alisema anachokifahamu Haji hakutendewa haki Simba naye atakuwa amekasirika kabla ya kuchukua hatua.

“Yule ni mtu mzima, anafahamu nini anafanya, naamini hajakosea kuondoka Simba wala hajakosea kujiunga Yanga,” alisema Sunday.


SIMBA WAJIBU

Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu alipoulizwa kuhusu Manara kutua kwa watani wao, alisema kwa ufupi; “Simba ni kubwa kuliko mtu yeyote sasa hapo ndipo wanasimba wataelewa nini CEO wetu Barbara Gonzalez alikuwa akikimaanisha, yeye keshatoka kwetu aende tu.”

Naye Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Ismail Aden Rage alisema; “Watu wanatakiwa wajue Haji hajaenda Yanga kama mwanachama ameenda kupiga kazi, hata wapinzani kwenye vyama vya siasa mpinzani hajawahi kumsifia mpinzani mwenzake.’

“Mimi namtakia mafanikio mema huko aendako kwani ameenda kutafuta riziki, ndio maana jana alikuwa smati sana kukataa kuulizwa maswali ni sahihi kabisa, nakubali sana kazi aliyoifanya Simba hivyo ngoja akatafute riziki, kwani kazi aliyoifanya Simba ndio hiyo anaenda kuifanya Yanga,” aliongeza Rage.

Mwanachama wa Simba, Justine Joel alisema kitendo alichokifanya Manara anajidhalilisha mwenyewe na kuonyesha wazi kuwa alikuwa msaliti hasa tuhuma zilizodaiwa kuwa anahujumu timu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad