Kauli ya IGP Sirro yazua gumzo





Baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro kuwataka askari kutokumuamini mtu, baadhi ya wachambuzi na wanaharakati wamesema kauli hiyo inaleta chuki kati ya wananchi na polisi.

Akiwa katika viwanja vya Polisi Kurasini juzi, wakati wa kuaga miili ya askari waliouawa kwa kupigwa risasi na Hamza Mohamed (30) katika shambulio lililotokea makutano ya Barabara ya Kinondoni na Kenyatta Drive, Sirro aliwataka askari kuongeza umakini wanapokuwa na silaha na hawatakiwi kumwamini mtu kwa kuwa sio watu wote wanawapenda.

“Huwa nawaambia siku zote, usicheze na mtu ovyo ovyo, usimuamini kila mtu, hii yote ni kwasababu ya imani. Walipomuona huyu Hamza walijua ni Mtanzania wa kawaida, kumbe alikuwa na silaha akawashambulia. Sisi askari tumeapa kufa kwa ajili ya kuwalinda Watanzania, lakini lazima Watanzania wajue na sisi tuna familia zetu,” alisema IGP Sirro.

Wakizungumzia hilo, wachambuzi hao walisema IGP anatakiwa atoe ufafanuzi kwasababu kauli hiyo inaweza kuleta taharuki.

Mratibu wa Mtandao wa watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa alisema kauli hiyo inapaswa kuangaliwa kwa mapana kwa sababu askari wanaishi na jamii, hivyo kuwa karibu na wananchi ni jambo ambalo haliepukiki.

“Ni kweli tupo kwenye majonzi ya vifo vya vijana wetu na Jeshi la Polisi limepoteza watu wake, lakini tunapaswa kuwa makini kuangalia kwa namna gani tunalichukulia suala hili, kauli ya kwamba askari wawe makini kwa watu wanaowasogelea, inapaswa kufanyiwa kazi kwa umakini, kwa sababu hilo ni agizo na askari wetu huwa wanafanya kazi kwa mujibu wa maagizo,” alishauri Olengurumwa.

“Tunashauri suala hili la Hamza lichukuliwe kama tukio la kihalifu kati ya matukio mengine yote na isionekane kwamba Watanzania wana tabia hiyo ya kuchukua silaha na kupiga askari. Hatuna matukio mengi tunayoweza kusema kwamba yametokea katika nchi yetu kwa mwaka huu, hata kwa miaka mitano au kumi iliyopita ambayo yameonesha askari wanapigwa na raia wanaokuwa nao karibu.”

Alisema tukio hilo lionekane kuwa ni la pekee na lisifanye askari kuanza kuwashughulikia raia wanaoishi nao kila siku.

Olengurumwa alisema wanakubaliana na kauli ya IGP Sirro kwamba askari wakati wote wawe waangalifu na wazingatie mafunzo yao waliyopewa wanapokuwa katika maeneo yao, lakini sio ya kutokumuamini kila mtu.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Anna Henga alisema kauli ya IGP Sirro ni kama inajenga kutokuaminiana.

“IGP aliongea kwa uchungu na kama amepaniki, lakini kauli hiyo inakuwa kama inachochea chuki kati ya askari na wananchi kwamba askari amuone kila mwananchi kwamba hampendi. Inajenga kutokuaminiana ambapo askari wanalinda usalama wa raia japo wanatakiwa wachukue tahadhari,” alisema Anna.

“Hivyo IGP angesema tu askari wachukue tahadhari na watumie elimu yao waliyofundishwa, lakini kauli aliyoitaka ni kama vile sisi hatuwapendi askari, kitu ambacho sio kweli. Ni kauli ambayo inatia huzuni, hakutakiwa kusema vile.”

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Bubelwa Kaiza alisema alichokifanya IGP Sirro ni kama analeta mazingira ya uadui kati ya polisi na wananchi, kitendo ambacho sio kizuri.

Alisema anachotakiwa kwasasa ni kuangalia mfumo na muundo wa jeshi hilo ili ubadilishwe na uendane na sasa.

“Kumekuwa na malalamiko polisi wanawaonea raia wasiokuwa na risasi au makosa yoyote. Amelalamika Rais, wamelalamika vyama vya siasa, wananchi, vyombo vya habari kwamba hawatendi haki, wananyanyasa watu bila kufuata taratibu na kuwaumiza. Hayo yote inatakiwa Jeshi la Polisi libadilike kimuundo na kimfumo, hayo yakishabadilishwa tutakuwa na jeshi jipya ambalo ni la huduma,” alisema Kaiza.

Mwanasaikolojia, Charles Kalungu alisema kauli ya IGP Sirro ina utata, kwani kuna watu watashindwa kuwaamini askari hivyo wataacha kwenda vituo vya polisi kutoa taarifa wakiamini siyo sehemu salama.

“Alichozungumza IGP kila mtu alielewa kulingana na upeo wake wa kifikra, unajua kuna baadhi ya mambo au kauli hazipaswi kabisa kusemwa waziwazi na kiongozi mwenye wadhifa mkubwa katika vyombo vya ulinzi na sekta nyinginezo kwa sababu kisaikolojia watu wengi huamini moja kwa moja kauli au uamuzi unaopitishwa na viongozi wakubwa bila kupinga japokuwa siku hizi upo mwamko mkubwa wa kifikra,” alisema.

 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad