Kenya imepokea dozi 880,000 ya chanjo ya Moderna kutoka Marekani Jumatatu asubuhi, kuimarisha mpango wa utoaji chanjo unaoendelea kote nchini.
Chanjo hizo ziliwasili uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta karibu saa kumi na mbili na robo, zinafuatia tangazo la Rais Joe Biden mapema mwaka huu kwamba that Washington DC itapeana dozi milioni 80 za chanjo kutoka kwa hifadhi yake.
Shehena hii ni sehemu ya dozi milioni 1.7 za chanjo zilizoahidiwa na Marekani kwa Kenya na zitawasilishwa kupitia mpango wa Gavi-Covax.
Kenya kufikia sasa imepokea dozi 3,610,100 za chanjo ya Covid-19.
Wiki iliyopita , nchi hiyo ilipokea msaada wa dozi 407,000 za chanjo ya AstraZeneca kutokaUingereza.
Mnamo mwezi Juni, Marekani iliorodhesha Kenya kuwa miongoni mwa nchi zitakazopokea dozi milioni 500 za chanjo ya Pfizer zitakazowasilishwa Agosti.
Kulingana na Wizara ya Afya, karibu watu 754,542 wamepokea dozi ya pili ya chanjo ya corona kufikia Jumanne wiki iliyopita.