Same. Mnyama kiboko aliyewaua watu wane kati ya mwaka 2017 hadi 2020 katika Kata ya Mabilioni wilayani Same mkoani Kilimanjaro na kuibuka hofu kubwa kwa wananchi wa Kata hiyo.
Miongoni mwa waliouawa na kiboko huyo ni wananume wawili na wanawake wawili katika mto Ruvu ambao wananchi hao huutumia kuchota maji kwaajili ya matumizi yao.
Akizungumza na Mwananchi Agosti 15, 2021 Diwani wa Kata hiyo ya Mabilioni, Lenard Kimweri amesema mnyama huyo ameendelea kuwa tishio kwa wananchi hao kwani amekuwa akionekana mara kwa mara pindi wananchi wakichota maji kwenye mto huo.
"Tuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji ndiyo maana huwa tunalazimika kuchota maji kwenye mto Ruvu ambao sasa sio salama kwani amejitokeza kiboko kwa takribani miaka minne sasa amekuwa tishio na ameshaua watu wanne tumekuwa hatuna amani kabisa," amesema Kimweri.
"Tunazo shule za msingi na sekondari na zote wanafunzi wanatakiwa kwenda na maji na huwa mara nyingine wanalazimika kwenda kuchota maji wenyewe kwenye mto kitu ambacho sio salama kwao kabisa," amesema Kimweri.
Kimweri amesema kutokana na changamoto hizo ametoa kiasi cha Sh6 milioni kwa ajili ya kuchimba maji kwenye eneo la shule ya sekondari Mabilioni kwani Shule hiyo ina wanafunzi wa kutwa na bweni ilikupunguza hatari kwa wanafunzi hao.
Mkuu wa Wilaya ya Same, Edward Mpogolo kufuatia changamoto ya mnyama huyo ametoa namba zake za simu kwa wananchi wa kata hiyo nakuwataka kutoa taarifa kwake pindi watakapo muona mnyama huyo amejitokeza.
Mpogolo amesema haiwezekani kumfumbia macho mnyama huyo ambaye ameua na anaendelea kuhatarisha maisha ya wananchi hivyo atahakikisha mnyama anatoweka mara moja kwenye eneo hilo sambamba na kuhakikisha changamoto ya maji inatatuliwa kwa wananchi wa Kata hiyo.
"Nimesikia changamoto zote hapa, ila hii ya kiboko niwaombe nipeni taarifa mapema munapo muona nipigieni simu muda wowote atakapokuwa amejitokeza," amesema Mpogolo.