Rais Joe Biden wa Marekani amesema ameidhinisha vikosi zaidi vya wanajeshi wa nchi yake kutumwa katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul, kusaidia ulinzi wa ubalozi wa Marekani na kuwaondowa wafanyakazi wake kutoka taifa hilo linaloelekea kuangukia mikononi mwa wapiganaji wa Taliban.
Biden amesema kutokana na ushauri wa wataalamu wa diplomasia, jeshi na ujasusi, ametoa idhini ya kutumwa wanajeshi 5,000 kuhakikisha usalama wa Wamarekani na washirika wao.
Katika tamko refu lililotolewa jioni ya jana, Biden ametetea uamuzi wake wa kuwaondoa wanajeshi wa Marekani kutoka Afghanistan, akihoji kwamba vikosi vya Kiafghani vinapaswa kupambana na wapiganaji wa Taliban wanaoendelea kuchukuwa maeneo kadhaa ya nchi.
Biden amesema Marekani waliwaambia Taliban kwenye mazungumzo ya Qatar kwamba kitendo chochote kitakachohatarisha maisha ya Wamarekani nchini Afghanistan kitajibiwa kwa hatua kali ya kijeshi.