Mamlaka ya viwanja vya ndege nchini Afghanistan ACAA imetangaza kufuta safari za ndege za kibiashara na kusema anga lake litatumiwa na ndege za kijeshi pekee hadi pale kutakapotolewa tangazo jingine.
Nchini Afghanistan hali inaonekana kuwa tete hasa baada ya wanamgambo wa Taliban kuuzingira mji mkuu wa taifa hilo Kabul. Mataifa mengi yameanza kuhamisha raia wao kutokana na hofu, huku mamlaka ya viwanja vya ndege nchini humo ACAA ikitangaza kufuta safari za ndege za kibiashara na kusema anga lake litatumiwa na ndege za kijeshi pekee, hadi pale kutakapotolewa tangazo jingine.
Mapema leo mamlaka ya anga nchini Afghanistan, ACAA ilitangaza kufunga eneo linalotumiwa na wasafiri wa kiraia kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa kimataifa wa Hamid Karzai uliopo mjini Kabul. Picha za video zilizosambaa zinaonyesha abiria waliofurika kiwanjani hapo wakivutana mashati, kila mmoja akitafuta angalau kijinafasi cha kujipitisha ili aingie kwenye ndege ya kijeshi iliyokuwa inawachukua watumishi wa ubalozi wa Marekani mjini Kabul.
Kulingana na ACAA, hatua hiyo inalenga kuzuia uporaji na uharibifu na kuonya abiria kutokimbilia uwanja wa ndege. Hata ndege zinazopitia Kabul nazo zimezuiwa.
Muda mfupi uliopita mashuhuda waliarifu kwamba watu watano wamekufa kwenye vuta nikuvute hiyo, huku wanajeshi wa Marekani wakiwa wameimarisha ulinzi wakati wakiwahamisha watumishi hao wa ubalozi. Haijajulikana iwapo waliuawa kwa risasi ama mkanyagano baada ya mashuhuda hao kusema mwanajeshi mmoja wa Marekani alifyatua risasi hewani ili kuwazuia abiria waliokuwa wakijaribu kulazimisha kuingia kwenye ndege.
Taliban yaahidi usalama kwa raia.
Jana usiku, rais Ashraf Ghani wa Afghanistan aliondoka nchini humo baada ya wanamgambo kuuzingira mji huo mkuu, baada ya kuidhibiti miji yote kwa siku kumi tu.
Muasisi mwenza wa kundi hilo Abdul Ghani Baradar amewatolea mwito wanamgambo hao kupitia mitandao ya kijamii akiwataka kuwa wenye nidhamu baada ya kuudhibiti mji huo mkuu. Amesema huu ndio wakati wa kuuhakikishia ulimwengu kwamba wanaweza kulitumikia na kuhakikisha usalama wa taifa lao, lakini pia mazingira bora ya kuishi.
Mjini Kabul, wanamgambo hao wameanza hii leo kukusanya silaha kutoka kwa raia kwa kuwa wamesema, hawatazihitaji tena kwa ajili ya kujilinda. Afisa mmoja wa Taliban ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba raia wanatakiwa wajue wako salama kwa sasa na kuongeza kuwa hawapo hapo kuwadhuru
Nchini Ujerumani, kansela Angela Merkel amesema serikali yake inajiandaa kupeleka wanajeshi nchini Afghanistan kusaidia kuwaondosha raia wake na WaAfghanistan wanaokabiliwa na kitisho kutoka kwa Taliban. Duru za bunge zimelimbia shirika la habari la AFP, zikimnukuu kansela Merkel alipozungumza na viongozi wa makundi ya ndani ya bunge kwamba serikali itaomba ridhaa ya bunge ili kukamilisha nia hiyo.
Jamhuri ya Czech pia imewaondosha watumishi wake na waziri mkuu Andrej Babis akisema watu 46 wamewasili Prague hii leo, huku Saudi Arabia nayo ikiripoti kwamba tayari imewahamisha wanadiplomasia wake. Serikali ya New Zealand kupitia waziri mkuu Jacinda Arden imesema inatuma ndege ya kuwachukua raia wake na watu waliowasidia, kuondoka nchini humo, na kutaja mikakati iliyofikiwa na baraza la mawaziri.
Amesema, "Wizara ya Mambo ya nje kwa sasa wanatathimini juu ya misaada kwa Waafghanistan walioathiriwa na mizozo. Msaada huu utakamilika baada ya kuthibitisha ni mashirika yapi ya kibinadamu yatakayofaa kutoa msaada kufuatia mabadiliko makubwa ya kiutendaji nchini Afghanistan."
Huku hayo yakiendelea, vikosi vya jumuiya ya kujihami, NATO na Uingereza vimesema haviterejea kupambana na wanamgambo hao nchini humo. Waziri wa ulinzi wa Uingereza Ben Wallace amekiambia kituo cha utangazaji cha Sky News kwamba anatambua Taliban wamerejesha udhibiti wake Afghanistan lakini kamwe hawatarejesha wanajeshi wake.
Amesema, wanachofanya sasa ni kuhakikisha raia wake na WaAfghnaistan wenye mahusiano nao wanaondolewa salama nchini humo. Italia yenyewe tayari imekwishawahamisha watumishi 70 wa ubalozi wake nchini humo. Ndege iliyowabeba iliondoka jana usiku na ilitarajiwa kufika Rome hii leo.