Dar es Salaam. Baada ya mtu kupata chanjo miongoni mwa mambo ya kuzingatia yanayosisitizwa ni kutopata kilevi cha aina yoyote kwa saa 72 sawa na siku tatu.
Wataalamu wa afya na watafiti wa chanjo wanasema pombe na dawa ya chanjo vyote vinakwenda kwenye ini, hivyo upo uwezekano wa ini kuongezewa mzigo na kulichosha lakini pia kilevi huingilia kazi ya dawa kama ilivyo kwa dawa zingine hivyo kupunguza ufanisi.
Mkurugenzi wa kuratibu na kukuza utafiti kutoka Taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu (NIMR) Dk Paul Kazyoba amesema kilevi cha aina yoyote hakitakiwi baada ya kuchanja kwani kitaingilia mfumo wa uzalishaji wa kinga za mwili ambao unafanywa na chanjo kwa saa za mwanzo.
Dk Kazyoba amesema chanjo inapochomwa katika mwili wa binadamu, ikiingia inaenda kuzisisimua seli za kinga ‘antibodies’ zinazalishwa zikishajaa mwilini zinakua askari wa kupambana na kirusi kitakachoingia.
Mambo ya kufanya kabla na baada ya kupata chanjo ya corona
“Kuufanya mwili uzalishe hizi seli kinga, inatakiwa usiingiliwe na kitu chochote cha tofauti kwenye damu kwa saa 72. Kilevi cha aina yoyote kwa maana ya pombe, bangi, shisha au dawa za kulevya lazima kitaingilia mfumo na hivyo kuifanya chanjo kutofanya kazi yake vizuri.
“Ndani ya saa 72 ni muda ambao kazi kubwa inafanyika hapo na ndiyo maana maudhi madogo madogo mtu anayapata ndani ya huo muda, vilevi vitaathiri uzalishaji wa mwanzo wa seli za kinga, ambazo zitajitengeneza mwilini mwako kwa miezi kadhaa,” amesema Dk Kazyoba.
Kitu kingine ambacho amekisema ni mwili kuutayarisha kabla ya chanjo ambapo alisema ni muhimu mwili ukawa na sawa na wenye nguvu za kutosha.
“Muda huo unaingiza kitu kipya mwilini, unaposhtuka na kuanza kupata uchovu na maudhi pale ndiyo unazalisha seli kinga kuuandaa mwili ili adui akijaribu kuingia akutane na kinga muda huo kama ukiona maudhi yanazidi mtafute daktari japokuwa wanaopata hali hiyo ni wachache,” amesema.
Kati ya mambo ya kuzingatia baada ya kuchoma chanjo, inatakiwa mtu aushughulishe mwili kwa kipindi cha saa 72 za awali kwani kwa kufanya hivyo seli za kinga huzalishwa kwa wingi na huwa na manufaa zaidi tofauti na kinyume chake.