WAKALA wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) wameruhusu kuanza kutumika kwa Mabasi 70 yaliyoachiwa hivi karibuni na Serikali ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa la kuyaachia Mabasi hayo ili yasaidie kupunguza kero ya usafiri Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari katika karakana ya Jangwani kabla ya Mabasi hayo kuingia barabarani, Kaimu Mkurugenzi wa uendeshaji wa DART Mhandisi Dkt. Philemon Mzee alisema hatua ya kuyaruhusu mabasi hayo kuanza kutoa huduma imefikiwa baada ya taratibu zote za kisheria kukamilika ikiwemo kupatiwa leseni na Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri Ardhini LARTA, pamoja na kujaribiwa ubora wake na vyombo mbalimbali vya Serikali.
“Tumekuja hapa kuuambia umma wa watanzania na wakazi wa Dar es Salaam kwa ujumla kwamba Serikali yao sikivu chini ya uongozi wa Rais wetu Mh. Samia Suluhu Hassan imeruhusu kuanza kutumika kwa Mabasi haya 70 yaendayo kwa Haraka ili kupunguza adha iliyokuwa inawakabili kwa muda mrefu kutokana na uchache wa Mabasi” Alisema Dkt.Mzee.
Alisema Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka unaendelea kumsimamia mtoa huduma ili afuate taratibu na kanuni zote za kuendesha mradi huo wa Mabasi Yaendayo Haraka ili adhma ya Serikali ya kuwapunguzia kero ya usafiri wakazi wa Dar es Salaam itimie.
Alisema kuanza kutumika kwa Mabasi hayo mapya 70 kutaleta unafuu wa usafiri katika Jiji la Dar es Salaam hasa katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa Uviko 19, ambapo wasafiri hawatakiwi kusongamana kwenye vyombo vya usafiri.
Awali Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliagiza kuachiwa kwa Mabasi hayo ili kusaidia utaoaji wa huduma ambazo zilizorota kutokana na uchache wa Mabasi katika mfumo wa Mabasi Yaendayo Haraka Jijini Dar es Salaam.
Aidha Waziri Mkuu aliwahi kuuagiza Wakala kuendelea kuboresha mradi huo kwani umekua kivutio kikubwa kwa wageni kutoka nje ya nchi ambao wanakuja kujifunza, jambo ambalo linailetea sifa Tanzania kwakua ni nchi ya kwanza katika Afrika Mashariki na Kati kuwa na mradi mkubwa kama huo.