WASANII wengi, hasa wa Bongo Fleva wanaoshinda ‘gym’ kwa ajili ya kutafuta mbavu nene (six packs), wanadaiwa kutumia dozi maalum ya kutanua miili, IJUMAA lina madai mazito.
Mastaa vinara Bongo wanaoongoza kwa kunyanyua vyuma kwa ajili ya kutengeneza mbavu nene na kuondoa vitambi na nyama uzembe ni pamoja na Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Rajab Abdul ‘Harmonize’ na msanii wake, Ibrahim Abdul ‘Ibraah’ Juma Mussa ‘Jux’, Emmanuel Mkono ‘Nahreel’, Mbwana Yusuf Kilungi ‘Mbosso’ na Nurdin Bilal ‘Shetta’.
Wengine ni Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’, Abdul Iddi ‘Lava Lava’, Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’ na wengine wengi.
Mbali na hao wa Bongo Fleva, pia wapo wa Bongo Movies kama Yusuf Mlela, Vincent Kigosi ‘Ray ’, Idriss Sultan, Burton Mwambe ‘Mwijaku’ na wengine kibao.
Baadhi yao wamesema kuwa, wanafanya hivyo ili kujiweka fiti na kuwa na mwili-jumba ili wasione aibu kuvua mashati wanapokuwa stejini.Hata hivyo, wakati mambo yakiwa hivyo, uchunguzi wa miezi kadhaa wa gazeti hili katika gym nyingi zinazotumiwa na mastaa mbalimbali jijini Dar; nyingi za Mbezi-Beach na Masaki, umebaini kwamba, mbali na kufanya mazoezi ya kunyanyua vyuma, lakini pia kuna kitu cha ziada kinachowafanya kutanuka mbavu ndani ya siku chache.
MWALIMU WA GYM
Mmoja wa walimu wa gym maarufu iliyopo Mbezi Beach jijini Dar ALIYEJITAMBULISHA KWA JINA LA Ticha Abbah amelithibitishia Gazeti la IJUMAA kwamba, mbali na mazoezi kuna dozi ya protini maarufu kwa jina la Whey ambayo hutumiwa na wengi kwa ajili ujenzi bora wa misuli na kuongeza nguvu wakati wa kufanya kazi nje.
“Ni sawa wanafanya mazoezi, lakini hawawezi kutanuka na kuwa na six packs kwa siku mbili au wiki moja. Mimi ninawajua vizuri, huyo Mondi na Harmonize kuna kitu kingine kinaitwa Whey.“
Pengine inawezekana lengo lao ni zuri tu kwamba wasiwe na vitambi na nyama uzembe ili waweze kupafomu vizuri jukwaani, lakini wengi wao wanataka kupata hiyo six pack kwa mkato ili wakivua mashati waonekane wapo vizuri kwamba ni watanashati.
“Ukweli ninaokuambia ndiyo uko hivyo, mastaa walio wengi wanataka waonekane wanajua kutunisha misuli au kupata maumbo ya miraba minne, lakini wamekuwa wakitumia dawa ili kuyapata maumbo hayo badala ya kufanya mazoezi ya viungo.
“Wasanii wengi hivi sasa wanatumia kwa wingi dawa hizo za kutunisha misuli kwa madai ya kuwa fiti kiulinzi binafsi na kuwa na pumzi wanapokuwa kwenye shoo zao, lakini vyovyote itakavyokuwa, najua tu zitakuwa na madhara kwa baadaye,” anasema Ticha Abbah.
WATAALAM
Hata hivyo, ili kupata ishu hiyo kinagaubaga, Gazeti la IJUMAA lilizungumza na wataalam mbalimbali wa afya ambapo walieleza wanachokifahamu juu ya dawa hizo za kutanua misuli.“Dawa za steroids za kuongeza ukubwa wa misuli ni kemikali zinazohusiana na homoni za kiume (tetosterones).
“Dawa hizo huchochea kukuza misuli na kustawisha maumbile ya kiume. Wavulana wanapobalehe homoni hizo huongezeka na kubadilika hivyo kuchochea mabadiliko ambayo humfanya mvulana awe mwanamume.
“Nyingine ni creatine ambazo huuzwa katika hali ya ungaunga au poda na kama ilivyo steroids, dawa hii nayo hujenga misuli na kuondoa maumivu ya mwili na Human Growth Hormone; vichocheo ambavyo hukuza misuli ya mtu kwa wiki chache tu.“Dawa nyingine zenye nguvu na zinazotumiwa zaidi na wanaume wanaotaka kujenga misuli ni Optimal Stack, Precision Power, Estoforce Edge, Muscle Ex Edge na Muscle Rip Edge.
MADHARA
“Lakini kuna baadhi ya vijana hutumia dawa hizo kukuza misuli kwa haraka na wengi huzitumia kwa kiwango kikubwa kiasi cha mara 10 hadi 100 zaidi ya kile ambacho kinahitajika na hapo ndipo kunakuwa na madhara.“Madhara yanayoweza kuwakuta wanaotumia vidonge vya vichocheo au steroids ni pamoja na maradhi ya moyo, lehemu mbaya mwilini, chunusi, upara, mabadiliko ya utendaji kazi wa moyo, ini na figo huweza kuharibika.
“Wengine huweza kupata matiti kama ya mwanamke. Mengine ni kukosa uwezo wa tendo la ndoa, kusinyaa au kupotea kwa korodani, tezi dume kukua, kuwa na hasira na shinikizo la damu.“Madhara mengine ni ogani muhimu kushindwa kufanya kazi ghafla, kama vile ini.
Kifo cha ghafla, saratani na figo kushindwa kufanya kazi.“Lakini pia, wataalam wanasema wengi wanaotumia dawa hizi hugeuka kuwa jeuri na wenye hasira za haraka hivyo siyo jambo la kulizoea kwa sababu uraibu wake ni mbaya mno,” anasema Dk Abdallah Mandai.Hata hivyo, Dk Mandai anaongeza kwamba, misuli ya mtu anayetumia dawa hizo inakuwa si imara kama ya mtu anayefanya mazoezi asilia.
VIFO
Ripoti mbalimbali ambazo IJUMAA limeziperuzi zinaonesha kuwa, vipo vifo kedekede ambavyo vilisababishwa na dawa za kutunisha misuli.
MAMLAKA
Hata hivyo, Gazeti la IJUMAA lilibisha hodi kwenye Mamlaka ya Chakula na Vifaa Tiba (Tanzania Medicines and Medical Devices Authority -TMDA) kuomba kuonana na msemaji wake, Gaudensia Simwanza ambaye hakupatikana.
Mmoja wa maofisa wake ambaye hakutaka kutajwa kuwa siyo msemaji, alisema dawa za kutunisha misuli zinaingia nchini kwa utaratibu wa uingizaji wa dawa na kabla ya kusajiliwa hupitia maabara na kupimwa.
Aliongeza kuwa, dawa hizo zinapotumika bila kuandikiwa na daktari na kutumiwa kiholela, huweza kusababisha madhara ingawa zikitumika kwa sababu husika madhara ni madogo, lakini zikitumiwa kwa sababu nyingine husababisha madhara