Mwanamke mmoja huko California amemuokoa mtoto wake wa miaka mitano kutoka kwenye shambulio la simba wa mlima.
Mtoto huyo alikuwa akicheza nje ya nyumba yake huko Calabasas katika milima ya Santa Monica, magharibi mwa Los Angeles, simba alipomshambulia.
Mtoto aliburuzwa kwenye nyasi, lakini mama yake alikimbia nje na kumpiga simba kwa mikono yake mpaka akamuacha mtoto wake.
Mnyama huyo alipatikana baadaye na kupigwa risasi na maafisa wa wanyamapori.
Mtoot alipata majeraha kichwani na mwilini, lakini sasa yuko katika hali nzuri katika hospitali huko Los Angeles, shirika la habari la Associated Press linaripoti.
Kapteni Patrick Foy, msemaji wa idara ya samaki na wanyama pori ya California, aliiambia AP kwamba mama huyo "ameokoa maisha ya mtoto wake".
Uchunguzi wa DNA baadaye ulithibitisha kuwa mnyama huyo ndiye aliyemshambulia mtoto.
Mashambulio ya simba wa milimani ni nadra sana Amerika Kaskazini.
Maafisa walisema mnyama aliyehusika alikuwa mchanga. Wataalam wanaamini kwamba alikuwa bado anajifunza jinsi ya kuwinda na kujitunza mwenyewe, kwa mujibu wa CBS News.