TUKIO la mauaji ya askari mkoani Dar es Salaam limeendelea kuibua utata, huku majirani na uongozi wa eneo alikokuwa anaishi anayedaiwa kuyatekeleza, wakisimulia maisha ya kijana huyo.
Baadhi ya majirani, akiwamo Venance Kalunga, katika mazungumzo na Nipashe jana, alidai kuwa juzi asubuhi walikuwa na kijana huyo maeneo ya nyumbani huko Mtaa wa Mataka na Senegal, Kata ya Upanga jijini.
Alidai kuwa wakiwa kwenye maeneo hayo, walikunywa kahawa na katika mazungumzo yao, kijana huyo alikuwa na malalamiko aliyotoa kwamba alikuwa na msongo wa mawazo.Kalunga alisema amemfahamu kijana huyo aliyemtaja kwa jina la Hamza tangu mwaka 1991, yaani miaka 20 iliyopita.
“Alikuwa mtu mwadilifu na utukutu alikuwa nao lakini haukuwa wa kutumia silaha wala wizi, sikuwahi kujua kama anamiliki silaha, wala sijajua ameitoa wapi. Ninachofahamu Hamza alikuwa anafanya kazi mgodini.
“Inawezekana alipata silaha baada ya kupata mali, mara ya mwisho kuonana naye ilikuwa jana (juzi) asubuhi, alisema ana msongo wa mawazo, wakati huo alikuwa anakunywa kahawa, kuna wazee huwa anakaa nao asubuhi, alikuwa anasema 'leo nina msongo wa mawazo isivyo kawaida'," alidai.
Kalunga alidai kuwa baada ya kunywa kahawa majira saa mbili asubuhi wakati watu wanakwenda kazini, alirudi kwao na baadae akaona kwenye mitandao ya kijamii tukio hilo alilolifanya.
“Sijawahi kuiona silaha yake, mara nyingi huwa katika migodi yake, miezi kadhaa iliyopita alirudi kutoka Misri.
Alivyorudi aliingia mgodini, akauendesha, akafanikiwa akanunua gari na pikipiki, akipata fedha akija anatuambia jamani kunyweni kahawa," alisema.
Alidai kuwa hata juzi wakati wanakunywa kahawa, waliamini amefanikiwa kama kawaida yake, lakini tukio lilivyotokea walishangaa.
"Tulishangaa, maadili hayo ameyatoa wapi? Na kwa nini anafanya hivyo? Wito wangu kwa vijana hata kama unakwazwa kwenye uendeshaji magari, labda trafiki amekukwaza, usitumie hasira au silaha kuumiza.
“Kwa Jeshi la Polisi wawe makini, uhifadhi na umiliki silaha wakati wakiwa lindo, tumeona jana (juzi) silaha tatu zimetumika pale, silaha ndogo na mbili zilizotoka kwenye vibanda vya polisi," alisema na kulishauri jeshi hilo lisimilikishe silaha watu ambao wana chembechembe za kuwa na matatizo ya akili.
“Hamza alikuwa na aina ya utukutu uliozidi ila ilikuwa kipindi cha nyuma kidogo, kuna kipindi aliruka ghorofani pale kwao akavunjika mguu.
Kwa hiyo pale ana ulemavu wa mguu," alidai.
Alidai mama yake alikuwa anajua ni mtukutu na hicho ndicho kinaaminika kuwa sababu ya kupelekwa Misri kufanyiwa dua.
Diwani wa Upanga Magharibi, Adnan Kondo, aliiambia Nipashe jana kuwa walipokea kwa mshtuko taarifa za tukio hilo, akibainisha kuwa kijana huyo alikuwa anaishi na mama yake na ni mkazi wa muda mrefu wa eneo hilo.
“Kwa tabia hakuwa na tabia nzuri, lakini hatukumjua sana kama tayari alishawahi kumpiga mtu au la, sijasikia kijana ambaye anamsifu kwamba alikuwa na tabia nzuri, sijasikia jirani ambaye anasema alikuwa na tabia nzuri, hili sijapata kusikia,” alisema.Kiongozi huyo alitoa wito kwa wananchi wa eneo hilo kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi endapo watatakiwa kutoa taarifa zozote kuhusu kijana huyo, akikiri kuwa tayari viongozi wa eneo hilo, akiwamo yeye, wamehojiwa na jeshi hilo kuhusiana na tukio hilo.
HALI ZA MAJERUHIMkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Aminiel Aligaesha, alisema jana kuwa walipokea majeruhi watano juzi kuanzia majira ya saa saba mchana wakiwa na majeraha makubwa na wengine madogo.Aligaesha alisema wanne kati yao ni askari wa Jeshi la Polisi na mmoja ni mlinzi wa kampuni binafsi ya SGA.
"Mara tu baada ya kupokewa, askari wawili mwenye umri wa miaka 41 na mwingine miaka 49, walikuwa na majeraha makubwa katika sehemu mbalimbali za mwili na ya viungo vya ndani, hivyo kufanyiwa upasuaji wa haraka ambapo upasuaji ulienda vizuri," alisema. Alisema askari wa tatu mwenye umri wa miaka 35, alipata majeraha makubwa na madogo katika maeneo ya mikono na mgongoni.
Alipewa huduma stahiki na kufungwa vidonda. Alisema mwingine mwenye miaka 46 alitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani kwa kuwa alikuwa na majeraha madogo.
“Mlinzi wa SGA miaka 42, alikuwa na majeraha ambayo hayakuhitaji upasuaji. Hata hivyo, alilazwa wodini jana (juzi) na ameruhusiwa leo (jana) kwenda nyumbani kuendelea na matibabu akiwa nyumbani,” alisema.
Aligaesha alisema wamebakiwa na majeruhi watatu ambao wanaendelea kupata matibabu na hali zao zinaendelea kuimarika.Pia alisema walipokea mwili wa mtu mmoja kutoka kwenye tukio hilo ambaye alikuwa ni mlinzi wa SGA na umehifadhiwa chumba cha kuhifadhi maiti.
Katika tukio hilo ambalo kiini chake bado kiko gizani, watu watano walifariki dunia akiwamo kijana huyo, askari watatu wa Jeshi la Polisi na mmoja wa Kampuni ya SGA.*Imeandaliwa na Romana Mallya na Kalebo Mussa (TUDARCo)