Kampuni ya Mawasiliano ya simu za mikononi ya Vodacom Tanzania imemteua Sitholizwe Mdlalose, kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo akichukua nafasi ya Hisham Hendi, ambaye alitangaza kujiuzulu na ukomo wa nafasi yake utafikia Novemba Mosi, 2021.
Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom aliyejiuzulu Hisham Hendi na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji mpya Sitholizwe Mdlalose
Taarifa ya uteuzi huo imetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Vodacom Tanzania Plc, Jaji (Mstaafu) Thomas Mihayo na kusema kwamba Sitholizwe Mdlalose, alikuwa ni Mkurugenzi wa Fedha wa Vodacom nchini Afrika Kusini na ana uzoefu wa zaidi ya miaka 19 kwenye sekta ya fedha, miaka 6 ikiwa ni ya nafasi za juu za uongozi katika sekta hiyo ndani ya Vodacom.
Mdlalose ana elimu ya Shahada ya kwanza ya Sayansi ya Uhasibu (BCompt) kutoka Chuo Kikuu cha Afrika Kusini, pia ni mtaaluma wa Uhasibu anayetambulika kimataifa (ACCA), ambapo pia ni mhitimu wa kozi ya juu ya uongozi kutoka shule kuu ya biashara, Chuo Kikuu cha Harvard.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa uteuzi wake unaakisi jitihada za Bodi ya Vodacom Tanzania yenye lengo la kusimika nafasi yake kwenye sekta ya mawasiliano nchini Tanzania.