Mhubiri mzaliwa wa Kenya anayeishi Uingereza amefikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa kuuza kile alichokiita 'dawa' ya Covid-19.
Askofu Irungu Wiseman wa kanisa la Bishop Climate aliuza chupa zenye mchanganyiko wa mafuta moja ikiwa ni pauni 91.
Alishtakiwa katika mahakama moja mjini London kwa udanganyifu na makosa ya ukosefu wa utendaji haki katika biashara.
Hata hivyo, alikanusha mashitaka hayo.
Bwana Wiseman alitengeneza video na kuzisambaza mtandaoni akidai mafuta hayo ni tiba ya Covid-19.
Hadi kufikia sasa, hakuna tiba ya Covid-19, kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).
Bwana Wiseman anaendesha kanisa la Bishop Climate Ministries ambalo ni sehemu ya Kanisa la Kingdom Church lililoko London Kusini.