Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), David Mataka amehukumiwa kwenda jela miaka minne ama kulipa faini ya Tsh milioni 8 baada ya kukutwa na hatia katika mashtaka waliokuwa wakikabiliwa nayo.
Hukumu hiyo imetolewa leo Ijumaa, Agosti 20, 2021 na Hakimu Mkazi Mkuu Janeth Mtega katika Mahakama ya Kisutu ambapo pia Mahakama hiyo imewahukumu watuhumiwa wenzake ambao ni Ramadhani Mlinga Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), na aliyekuwa mwanasheria wa mamlaka hiyo, Bertha Soka kifungo cha mwaka mmoja ama kulipa faini ya Tsh milioni 2 kila mmoja.
Mattaka na wenzake walikuwa akikabiliwa na mashitaka sita likiwemo la matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 71. Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi zaidi ya 20 na vielelezo.
Ilidaiwa mahakamani kuwa, Oktoba 9 mwaka 2007 wakati Mattaka akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, alitumia madaraka vibaya kwa kusaini mkataba wa kukodisha ndege aina ya Airbus na kwamba mkataba huo unadaiwa kuisababishia serikali hasara ya zaidi.
Katika shitaka lingine Dk Mlinga na Soka walidaiwa kuwa Machi 19, 2008 katika ofisi za PPRA Ilala, Dar es Salaam walighushi muhtasari wa kikao wa tarehe hiyo, wakionesha kwamba mamlaka hiyo ilikaa kikao na kujadili maombi ya kuidhinisha ATCL ikodishe ndege hiyo.