Mshitakiwa kesi ya Sabaya adai ‘imepikwa’
MSHITAKIWA wa tatu katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro Lengai Ole Sabaya (34) na wenzake wawili, Daniel Mbura (38) amedai kuwa mashitaka dhidi ya yake ni ya uongo, uonevu na ‘yamepikwa’
Mbura jana aliiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha imfutie mashitaka hayo. Alisema hayo mahakamani wakati akiongozwa na wakili wake, Fridolini Gwemelo mbele ya Hakimu Mwandamizi Odira Amworo.
Mbura alidai kuwa, Februari 9 mwaka huu siku nzima alikuwa nyumbani akiendelea na shughuli zake na hakutoka hivyo hafahamu chochote kuhusu tukio hilo, hamfahamu Sabaya na pia hamfahamu mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo Silvester Nyengu (26).
Mbura alidai kuwa Polisi hawahawahi kumkamatwa ila aliwahi kupigiwa simu na shahidi wa tisa katika kesi hiyo, Evarest Mwamengo Februari 16 mwaka huu kuwa anahitajika kituo Kikuu cha Polisi Arusha.
Alieleza mahakama kuwa alienda lakini aliambiwa akihitajika atatafutwa tena na Juni 3 mwaka huu Mwamengo alimpigia tena kumhitaji polisi na Juni 4 mwaka huu alifikishwa mahakamani kwa shitaka linalomkabili sasa.
Alidai kuwa kielelezo kilichopelekwa mahakamani hapo cha gwaride la utambuzi la kinachoweza kutengenezwa na mtu yoyote hivyo hakitambui.
Mbura aliendelea kudai mahakamani kuwa yeye anaitwa Daniel Laurent Mbura na si Daniel Gabriel Mbura kama ilivyoandikwa kwenye hati ya mashitaka, ana umri wa miaka 31, anaishi Shams jijini Arusha.