Mmoja wa wasichana wa shule nchini Nigeria waliokamatwa na wanamgambo wa Kiislamu Boko Haram kutoka mji wa Chibok mnamo mwaka 2014 ameachiliwa huru na kujiunga tena na familia yake.
Ruth Ngladar Pogu na mwanaume ambaye anasemekana alimuoa akiwa ameshikiliwa mateka, hivi karibuni walijisalimisha kwa jeshi la Nigeria, kulingana na maafisa.
Wanandoa hao wana watoto wawili.
Zaidi ya wasichana 270 walitekwa nyara huko Chibok, kaskazini mashariki mwa jimbo la Borno.
Zaidi ya wasichana hao 100 wameachiwa huru au wamefanikiwa kutoroka.
Lakini wengine bado hawajulikani walipo.
Ruth Ngladar Pogu na watoto wake walipokelewa na gavana wa jimbo la Borno, maafisa hao walisema.
Walisema sasa atakuwa akiendelea na mpango wa kurekebisha tabia na kuungana tena na jamii ambao utazingatia afya yake na ustawi wa kisaikolojia.
Kati ya mamia ya wasichana waliotekwa nyara kwa mara ya kwanza, wengine walifanikiwa kutoroka muda mfupi baada ya kukamatwa, wakati karibu 100 waliachiliwa huru katika mabadilishano ya wanamgambo wengine wa Boko Haram.
Utekaji nyara umesalia kuwa tatizo kaskazini mwa Nigeria, huku mamia ya wanafunzi wakitekwa mwaka huu pekee.