MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ilionesha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limejiendesha kwa hasara lakini hakusema lifutwe.
Msigwa amezungumza hayo mapema leo alipokuwa akifanya mahojiano maalum na Kipindi cha Front Page kinachorushwa kupitia +255 Global Radio ambapo alifafanua masuala mbalimbali yanayoihusu Serikali.
Alisema, ni kweli Shirika la Ndege lilijiendesha kwa hasara lakini haimaanishi kwamba shirika hilo halijatoa faida katika maeneo mengine ya kiuchumi.
CAG hakusema Shirika la Ndege halifai isipokuwa hesabu, wataalam wa mahesabu wanajua, hakuna nchi inayopata faida kwa kuuza tiketi za ndege. Faida inapatikana katika maeneo mengine ya kiuchumi kama utalii. Tukikosa watalii tunakosa pesa, ukileta ndege ndipo utaona faida ya utalii,” alisema Msigwa.
Akizungumzia vitambulisho vya mjasiriamali, Msigwa alisema Serikali inakwenda kuviboresha na vitakuwa na hadhi ya kuwawezesha wajasiriamali kuweza hata kupewa mikopo kwa kupitia vitambulisho hivyo.
“Mhe Rais Samia Suluhu ameshasema vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo vitaboreshwa kwa kuongezewa taarifa na kuwekwa kwenye kazi data ili hata taasisi za fedha mfano mabenki wawe na uhakika na huyu mfanyabiashara na anaweza hata kukopeshwa,” Msigwa.
Msigwa alitumia nafasi hiyo pia kuwazungumzia wasanii wa Bongo Fleva na Bongo Muvi kuwa wanafanya kazi nzuri, na Serikali ipo pamoja nao katika kuhakikisha wanafanya shughuli zao vizuri.
‘Bongo Muvi kidogo iliyumba lakini kwa sasa nao wamekuja vizuri. Tunawapongeza kwa kweli wanatumia nguvu zao kufanya vizuri na sasa hivi hata ukiwauliza Afrika Mashariki wasanii wa muziki wanaofanya vizuri utakuta wote wanatokea Tanzania,’ alisema Msigwa.
Stori: Erick Evarist