Waendesha mashtaka nchini Libya wametoa waranti ya kukamatwa kwa Saif al-Islam Gaddafi, mtoto wa aliyekuwa kiongozi wa Libya marehemu Muammar Gaddafi, juu ya tuhuma za uhusiano na mamluki wa Urusi.
Uchunguzi wa BBC umebaini uhusiano kati ya shughuli za kikundi cha Wagner huko Libya na uhalifu wa kivita uliofanywa dhidi ya raia wa Libya.
Wapiganaji wa Urusi walionekana kwa mara ya kwanza nchini Libya mnamo 2019 walipojiunga na vikosi vya jenerali muasi, Khalifa Haftar, kushambulia serikali inayoungwa mkono na UN katika mji mkuu Tripoli. Mzozo huo ulimalizika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano mnamo Oktoba 2020.
Kikundi cha Wagner kiligunduliwa kwa mara ya kwanza mnamo 2014 wakati kilikuwa kikiunga mkono wapiganaji wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Urusi katika mzozo mashariki mwa Ukraine. Tangu wakati huo, kundi hilo limehusika katika mizozo ya Syria, Msumbiji, Sudan, na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Amri ya kukamatwa kwa Saif al-Islam Gaddafi ilisambazwa ndani kwa vyombo vya usalama vya Libya na mwendesha mashtaka Mohammed Gharouda mnamo 5 Agosti, lakini ilitangazwa kwa umma tu baada ya uchunguzi wa BBC .