Mvua ya upepo na barafu iliyonyesha wilayani Biharamulo Mkoa wa Kagera juzi imeharibu mazao na nyumba na kuacha barafu katika makazi.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Jumamosi Agosti 14, 2021 Diwani wa Biharamulo Mjini, David Mwenenkunda amesema mvua hiyo iliyonyesha jana jioni kuanzia saa nane mchana hadi saa kumi jioni imeacha madhara kwa wakazi wa kata hiyo nyumba zao kuharibika kwa kujaa maji na barafu.
"Mpaka sasa upepo ulikuwepo lakini hakuna nyumba iliyoezuliwa, zimetoboka kwenye kuta kwa sababu ya mawe ya mvua,"amesema Mwendankunda.
Ametaja maeneo yaliyoathirika ni mitaa ya Lubondo na Lukaragata ambayo mpaka sasa barafu bado hazijayeyuka kuisha licha ya uwepo wa jua.
Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo Kemilembe Lwota amesema mvua hiyo imenyesha na baada ya wananchi kutoa taarifa ametembelea maeneo yaliyoathiriwa na mvua hiyo.
Amesema mvua hiyo haijasababisha madhara makubwa kwa wananchi zaidi ya kuwepo barafu kwenye maeneo yao.
Shuhuda wa tukio hilo Sadoth Trazias amesema lilikuwa tukio la kushangaza kutokana na mvua hiyo.