Mwanaume mmoja aliyetishia kuripua bomu kwenye viunga vya majengo ya bunge nchini Marekani amejisalimisha kwa polisi na kuhitimisha saa kadhaa za taharuki katika mji mkuu wa taifa hilo wa Washington.
Mtuhumiwa huyo aliyetambuliwa na maafisa wa usalama kama mfuasi wa siasa kali amejisalimisha baada ya kutishia kwamba angeripua bomu kutoka kwenye gari alilokuwemo na ambalo aliliegesha karibu na majengo ya bunge la Marekani.
Mwanaume huyo Floyd Roseberry alitumia mtandao wa kijamii kurusha tukio hilo moja kwa moja huku akitoa matamshi ya kumkashifu rais Joe Biden wa Marekani na kukosoa sera ya taifa hilo kuelekea Afghanistan.
Hata hivyo maafisa wa usalama hawakukuta bomu katika upekuzi waliofanya baada ya kumalizika kwa taharuki hiyo iliyolazimisha watu kuhamishwa na mamia ya polisi kutumwa kwenye eneo la tukio.