NAIBU Waziri wa Kilimo Hussein Bashe,amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt Philemon Sengati kuyaachia zaidi ya magari 30 yaliyokuwa yamebeba zao la Dengu kuyazuia kwa madai ya kukiuka masharti ya stakabadhi ghalani.
Agizo hilo amelitoa leo Agosti 27,2021 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari amesema kuwa kuanzia leo magari yote yaliyokamatwa katika mkoa wa Shinyanga yaachiwe mara moja.
“Agosti 10 mwaka huu,nilipata malalamiko kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi kutoka kwa wafanyabiashara wa mazao wa mikoa ya Mwanza na
Mara,wakilalamikia kukamatwa kwa magari yao katika Mkoa wa Shinyanga
na kulazimishwa kufuata utaratibu wa kuuza mazao hayo kwa mfumo wa
stakabadhi ghalani.”amesema Bashe
Ameongeza kuwa baada ya kupokea malalamiko hayo alimuandikia ujumbe mfupi kwa njia ya simu Mkuu wa Mkoa Shinyanga Sengati na kumtaka kuwaachia na kuwaruhusu
kuendelea na utaratibu wao bado alikaidi, ndipo Agosti 20, mwaka huu nilimwandikia barua nikimueleza kuwa katika mikoa ya Shinyanga na baadhi ya mikoa mingine hakuna mfumo wa stakabadhi ghalani lakini aliendelea kukaidi.
Bashe amesema kuwa wafanyabiashara wana leseni lakini wanapofika katika mkoa wa Shinyanga wanakamatwa wakati mwenye Mamlaka ya kuagiza zao liuzwe kwa namna gani katika minada ni Waziri wa Kilimo pekee.
“Jambo hili haliwezekani,Wafanyabiashara wamelipa ushuru lakini wanakamatwa ,hatutaki namna hii jambo hili sio zuri”amesema Bashe
Hata hivyo ,Bashe amesema halitajirudia lililotokea Shinyanga huku akiwapa pole wakulima pamoja na wafanyabiashara waliopata kadhia hiyo.
“Niwahakikishie wakulima na wafanyabiashara wa Nchi hii Wizara ya Kilimo itaendeelea kuwalinda kwa nguvu zote kuhakikisha mazingira ya kufanya biashara yanakuwa rafiki,”amesema Bashe.