NI rasmi sasa kwamba, msanii kinara wa kike wa Bongo Fleva, Faustina Charles Mfinanga au Nandy ameshindika na hakamatiki kutokana na spidi ya mafanikio anayoyapata kila kukicha, Gazeti la IJUMAA lina ripoti kamili.
NANDY: HAKUNA KINACHOSHINDIKANA
Katika mazungumzo na Gazeti la IJUMAA, Nandy anasema kuwa, ukiamua kuweka ndoto zako za kusaka mafanikio, hakuna kinachoshindikana katika kuzitimiza na hicho ndicho kinachojiri kwa upande wake.Nandy anakiri kwamba, moja ya ndoto zake kubwa ilikuwa ni kumiliki ndinga kali na la kifahari aina ya Range Rover Evoque ambalo amejizawadia wiki mbili zilizopita.
“Lakini yote kwa yote, ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa hapa nilipofikia kwa kweli,” anasema Nandy ambaye ni binti mwenye umri wa miaka 28 tu kwa sasa, lakini ana mafanikio makubwa yanayowatoa kijasho hata midume kibao kwenye muziki wa Bongo Fleva.
Mbali na Range Rover Evoque ambalo badala ya kuweka nambari ya usajili ameweka jina lake, Nandy au The African Princess anamiliki magari mengi ya kifahari huku akiwa na muda mchache wa miaka takriban mitano tu kwenye gemu la Bongo Fleva ukilinganisha na wasanii wengi wenye zaidi ya miaka kumi kwenye muziki, lakini hawamfikii.
Baadhi ya magari mengine ya Nandy ya kifahari ni pamoja na Land Rover Discover TDV6 HSE, BMW X1, Mercedes Benz E-Class E320 CDI, Toyota Alphard, Toyota Harrier na Toyota Noah ambayo anayatumia kwa shughuli zake mbalimbali.
BAADA YA JIDE NI ZAMU YA NANDY
Baada ya tu ya kuonesha ndinga lake hilo jipya, kurasa mbalimbali za wachambuzi wa burudani kwenye mitandao ya kijamii zimemtangaza rasmi Nandy kuwa Bosi Lady mpya Bongo kutokana na kumiliki gari hilo ambalo linaaminika kwamba huwezi kuwa nalo kama akaunti yako ya benki inasoma chini ya shilingi milioni 100 na huna miradi zaidi ya mmoja ya kukuingizia pesa ndefu kila siku.
Mara ya mwisho, staa mwanamke wa Bongo Fleva aliyekuwa na gari la aina hiyo ya Range Rover Evoque ni mkongwe, mwanadada Judith Wambura au Lady Jaydee au Jide, lakini kwa sasa Nandy ndiye msanii pekee anayemiliki gari hilo jipya analodai ni toleo la mwaka 2020.
NANDY JESHI LA MTU MMOJA
Mitandao mbalimbali ya burudani Afrika Mashariki inamtaja Nandy kama binti mwenye mafanikio ya aina yake ukimlinganisha na warembo wanaofanya muziki wa Bongo Fleva kwa uwezo wa kimuziki pamoja na umiliki wa mali kwa maana ya kimafanikio akiwa ni jeshi la mtu mmoja tofauti na wengine walio chini ya lebo mbalimbali za muziki.
Gazeti la IJUMAA lilipotaka kujua siri ya mafanikio ya Nandy, mrembo huyo anasema kuwa, siri kubwa kuliko zote ni kujituma na kujiwekea malengo katika kazi zake.“Siri ya mafanikio yangu inatokana na juhudi zangu.
Pia nina menejimenti nzuri ambayo ipo siriazi sana linapokuja suala la kazi, ndiyo maana imenifanya niwe na mafanikio,” anasema Nandy ambaye jina lake la utotoni ni Nandera ambaye producer wake, Kimambo anasema kwamba, ni jambo kawaida kwa mrembo huyo kukesha studio akiandaa nyimbo nzuri ili akidhi kiu ya mashabiki wake wanaohitaji muziki wake mzuri.
MIRADI MINGINE YA NANDY
Licha ya Nandy kutoanika miradi yake mingine, lakini Gazeti la IJUMAA linafahamu ana kampuni ya bidhaa za urembo na pia hivi karibuni alipata ubalozi wa bia nchini Tanzania. Nandy pia siku za hivi karibuni amekuwa akiweka rekodi ya kujaza watu wengi kwenye shoo za uwanjani kupitia tamasha lake la Nandy Festival ambalo tayari kwa mwaka 2021 limepita mikoa kadhaa nchini Tanzania na kutikisa vilivyo.
UTAJIRI WA NANDY 2020
Kwa mujibu wa mitandao mbalimbali inayokadiria utajiri wa mastaa kwa upande wa Afrika Mashariki, mwishoni mwa mwaka jana (2020), Nandy alikadiriwa kuwa na utajiri wa Dola za Kimarekani milioni moja ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 2.3 za Kitanzania.Lakini ikumbukwe kwamba, utajiri huo unatokana na thamani ya muziki wake kwa maana ya mauzo na shoo, vitu vyote anavyovimiliki Nandy kuanzia kampuni, magari na nyumba kama anazo.
GPL