TIMU ya soka ya Geita Gold ya mkoani Geita iliyopanda daraja kucheza Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao, imemtambulisha aliyekuwa Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Ettiene Ndayiragije kuwa kocha wao mkuu huku yeye akiomba ushirikiano wa timu hiyo ambapo atasaidiana na kocha Fred Felix Minziro kuelekea msimu ujao wa ligi.Afisa habari wa timu hiyo, Aman Nichoraus ameliambia Championi kuwa: “Kocha Ettiene Ndayiragije amesaini mkataba wa kuinoa klabu yetu kwa muda wa miaka miwili ambapo atasaidiana na kocha aliyetupandisha daraja, Fred Felix Minziro ambapo tunaamini wataliongoza jahazi la Geita Gold kufanya vizuri kwenye ligi kuu.
“Sababu kuu za kumleta Ndayiragije ni uwezo wake aliouonyesha wakati akifundisha klabu za Tanzania kwani wote ni mashahidi kwamba wakati Ndayiragije alipokuwa kocha wa Mbao wote mliona ilivyokua ikifanya vizuri, alipoenda KMC timu ile ilibadilika na hata alipopewa kazi Azam FC bado kazi yake ilionekana kuwa kubwa mpaka kuitwa timu ya taifa hivyo sisi kaka Geita tunaamini atatusaidia.
’Kwa upande wake Kocha Ettiene Ndayiragije alisema: “Nawashukuru sana viongozi wa Geita kwa kuniamini na kunipa kazi sina cha kuwalipa ila nawaomba ushirikiano ili tuweze kuifanya Geita Gold kuwa timu bora.”