Arusha. Aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai Mkoa wa Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya amesema alinusurika kuuawa mara mbili akiwa katika wadhifa huo na kuwa mkimbizi kwenye nchi yake kutokana na sababu za kisiasa ghilba na chuki dhidi yake.
Akijitetea katika leo Agosti 16 Kesi ya unyang'anyi wa kutumia silaha inayomkabili yeye na wenzake wawili, Sabaya amesema kesi hiyo inayomkabili ni ya kutengeneza baada ya kushindwa kumfanyia jambo kubwa.
Mbele ya hakimu mkazi Mwandamizi Odira Amworo akiongozwa na mawakili wake Moses Mahuna na Dancon Oola, Sabaya amesema kwa wiki tatu alikuwa mkimbizi ndani ya wilaya yake na kuna watu walitaka kuondoa maisha yake na familia yake.
Amesema wakuu wa vyombo vya Dola wanajua na hata mamlaka za juu zilikuwa zinajua.
Amneendelea kusema kuwa, Polisi wamedanganywa na waendesha mashitaka wamedanganywa katika kesi hiyo kwani inatokana na siasa za Arusha na Hai.
Sabaya amesema katika kesi hiyo mashahidi wote wameshindwa kuthibitisha yeye kuiba fedha na ameomba Mahakama imtendee haki.
Katika shauri hilo la jinai namba 105 la mwaka 2021, upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu Tumaini Kweka, Mawakili wa Serikali Baraka Mgaya na Felix Kwetukia.
Utetezi uliwakilishwa na mawakili Mahuna, Oola, Edmund Ngemela, Fridolin Gwemelo na Jeston Jastin.
Katika kesi Hiyo, Sabaya wenzake, Sylivester Nyegu na Daniel Mbura wanashitakiwa kosa la kwanza unyang'anyi wa kutumia silaha na kujipatia kIasi cha 2.769,000 Million Mali ya Mohamed Saad Februari 9, katika duka lake lililo mtaawa bondeni jijini Arusha.
Kosa la pili ni la wizi wa kutumia silaha ambapo February 9, Sabaya na wenzake wawili wakiiba fedha Sh390,000 mali ya Bakari Msangi ambaye ni diwani wa CCM Kata ya Sombetini baada ya kumpiga na kumtishia kwa bunduki.
Shitaka la tatu Sabaya na wenzake Wanatumiwa kuiba Sh35,000 na simu aina ya Tecno, mali ya Ramadhani Rashid baada ya kumtishia kwa silaha na kumfunga pingu February 9 mtaa wa Bondeni katika duka hilo la Mohamed Saad.