Samia atumbua wakurugenzi 54
WIZARA ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imetoa siku tano kuanzia leo kwa wakurugenzi wapya wa majiji, manispaa, miji na halmashauri za wilaya wafi ke kwenye vituo vya kazi kuanza kutekeleza majukumu yao.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Ummy Mwalimu amewataka wakurugenzi hao waende kuripoti kwa makatibu tawala wa mikoa kwenye mikoa husika.
Rais Samia Suluhu Hassan juzi ameteua jumla ya wakurugenzi 184, na kwa mujibu wa Ummy, 70 kati ya hao wamehamishwa kutoka vituo vyao vya kazi na 45 wamebaki walipokuwa.
“Aidha, katika idadi hiyo wakurugenzi 69 ni wapya wakiwemo 15 walioteuliwa kujaza nafasi 54 zilizoachwa wazi baada ya waliokuwa wakurugenzi katika nafasi hizo kutenguliwa,” alisema Ummy alipozungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana. Ummy alisema miongoni mwa wakurugenzi wapya, 33 sawa na asilimia 48 ni wanawake na hivyo kufanya idadi ya jumla ya wanawake wakurugenzi kufikia 55 sawa na asilimia 29 ya wakurugenzi wote nchini.
Alisema wakurugenzi wawili ambao majina yameonekana kutokea kwenye maeneo zaidi ya moja wanapaswa kwenda kuripoti kwenye kituo ambacho jina limeonekana kwa mara ya kwanza kwenye orodha ya uteuzi.
Alisema pale ambapo jina limejirudia patatambulika kama nafasi wazi na itajazwa baadaye na akazitaja nafasi hizo ni Halmashauri ya Mji wa Misungwi na Njombe.
Ummy aliwataka wakurugenzi ambao uteuzi wao umetenguliwa waende kuripoti kwa makatibu tawala wa mikoa waliyokuwa wakivifanyia kazi ili wapangiwe majukumu mengine kwa kuwa bado ni watumishi wa umma.