SERIKALI ya Tanzania imesema, jumla ya wananchi wake 300,000 wamepata chanjo ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona (COVID-19). Anaripoti Patricia Kighono, TUDARCo … (endelea).
Chanjo hiyo aina ya Johnson & Johnson ambayo ni msaada kutoka Marekani, ilizinduliwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, tarehe 28 Julai 2021 huku akiwahamaisha wananchi kujitokeza kupata chanjo hiyo.
Tanzania ilipokea msaada wa chanjo hiyo milioni moja awamu ya kwanza na zingine, zinatarajiwa kuletwa katika siku za usoni.
Leo Ijumaa, tarehe 28 Agosti 2021, Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma amesema, wananchi wameendelea kujitokeza kwa wingi kupata chanjo hiyo.
Gerson Msigwa, Msemaji wa Serikali
“Tangu kuanza kwa zoezi hili la chanjo, Watanzania takribani laki tatu wamechanjwa,” amesema Msigwa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo
Amesema, “ugonjwa upo, Watanzania wanaugua, wanapata matatizo na wengi ni kwa sababu wamekataa kupokea chanjo. Tunawaomba tuwasikilize wataalamu wetu, wanavyotushauri.”
Msemaji huyo wa serikali amewasihi wananchi kuacha kusikia wapotoshaji kwani “ukiumwa ukapetewa hospitalini na kuwekewa mashine utakuwa wewe peke yako, tuwasikilize sana wataalamu wetu.”
Amesema, utaratibu unaandaliwa ili kuanza kuzunguka nchi nzima ikiwemo vijijini ili kusogeza karibu zaidi huduma hiyo ya chanjo