Mashambulizi ya Marekani ya ndege zisizo na rubani katika mji mkuu Kabul umezuia shambulio jingine baya la kujitoa uhanga katika uwanja wa ndege, maafisa wa jeshi la Marekani wamesema.
Shamulio hilo lililenga gari lililobeba takribani mtu mmoja anayehusishwa na kundi la Islamic State, tawi la Afghanistan, jeshi la Marekani limeeleza.
Marekani ilionya juu ya uwezekano wa mashambulio mengine wakati operesheni za kuondoa raia zikitamatika.
Pamoja na hayo, imesema kuwa itaendelea kuwaondoa Waafghan kutoka uwanja wa ndege wa Kabul hadi "saa za mwisho".
Tarehe ya mwisho ya ujumbe wa uokoaji ya Agosti 31 ilikubaliwa kati ya Marekani na Taliban, ambao sasa wanadhibiti sehemu kubwa ya nchi.
Marekani itakuwa ya mwisho kumaliza kazi yake, na nchi nyingine zote tayari zimekamilisha zao.
Ndege za mwisho zinazowarudisha wanajeshi wa Uingereza kutoka Afghanistan zimekuwa zikiwasili nchini Uingereza siku ya Jumapili.
Marekani inasema imewezesha uokoaji wa watu zaidi ya 110,000 kutoka uwanja wa ndege wa Kabul tangu tarehe 14 mwezi Agosti - siku moja kabla ya Taliban kuchukua udhibiti wa mji mkuu.
Mwandishi wa BBC Lyse Doucet, huko Kabul, anasema yeye na wenzake bado wanapokea ujumbe wa dharura wa SOS kutoka kwa Waafghan ambao wanahisi kutishiwa na Taliban. Wao ni pamoja na wanamuziki, wanafunzi wa vyuo vikuu na wanasiasa wa kike.
Wengi wao wanahisi hawawezi kuwa na mustakabali waliojiandaa nao baada ya miongo miwili ya ushiriki wa kimataifa, mwandishi wetu anasema - na wengi wanasema Taliban wanawazuia kuondoka.
Siku ya Jumapili, Kapteni Bill Urban alisema Marekani ilifanya mashambulizi lililolenga "kuondoa tishio karibu" na uwanja wa ndege wa Kabul.
"Tuna imani tumefanikiwa kufikia lengo," alisema, na kuongeza: "Milipuko ya pili kutoka kwenye gari ilionesha uwepo wa idadi kubwa ya vifaa vya kulipuka."
Alisema baadaye kwamba jeshi lilifahamu ripoti za majeruhi za raia kufuatia shambulio la ndege isiyo na rubani. "Haijulikani ni nini kinaweza kuwa kimetokea, na tunachunguza zaidi," alisema, akiongeza kuwa "wanasikitishwa sana na upotezaji wowote wa maisha ya wasio na hatia".
Maoni yake yalikuja baada ya ripoti nyingi za mlipuko mkubwa uliosikika karibu na uwanja wa ndege wa Kabul. Picha nyigine zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zilionesha mawingu meusi ya moshi yanayopanda hewani juu ya majengo.
Maafisa wa ujasusi wa Marekani mapema walisema wamepokea vitisho '', vya kuaminika" dhidi ya uwanja wa ndege, na kwamba wanajeshi wataendelea kutekeleza mashambulizi pale inapobidi.
Marekani ilishauri watu kukaa mbali na eneo hilo, licha ya muda kuisha kwa mtu yeyote anayejaribu kupata ndege za uokoaji.
Kando na hayo, Jumapili, polisi wa Kabul walisema mtoto alikuwa ameuawa katika shambulio la roketi kwenye nyumba karibu na uwanja wa ndege. Maelezo kuhusu shambulio hilo hayajawekwa wazi.
Shambulio la bomu katika uwanja wa ndege Alhamisi iliyopita liliua watu 170, pamoja na wanajeshi 13 wa Marekani.
Kundi la , IS-K, lilikiri kutekeleza shabulio la Alhamisi.
Kwa kulipiza kisasi, Marekani ilifanya mashabulizi ya ndege zisizo na rubani mashariki mwa Afghanistan Ijumaa, ikisema imeua wafuasi wawili "wa juu" wa IS-K.
Rais wa Marekani Joe Biden Jumapili alikutana na familia za wafanyikazi 13 wa Marekani waliouawa katika shambulio la uwanja wa ndege wa Kabul Alhamisi.
Bwana Biden alishiriki katika hafla ya heshima kwa waathiriwa katika kituo cha Jeshi la Anga la Dover huko Delaware.