Simba mafia sana! Yaipora beki Yanga, afichwa Dar



 
KWA lugha za kwenye vibanda umiza ni kwamba Yanga wamebipu, Simba wakapiga kweli. Hivi karibuni kulikuwa na tetesi kwamba Yanga imenasa kiungo, Peter Banda aliyekuwa anakwenda Simba na kuwafanya kuhaha kwa saa chache wakimsaka kumrejesha kwenye himaya yao kabla ya juzi mchana kumsainisha Msimbazi.

Kitendo hicho kiliwakera Simba na wakaanza kejeli mitandaoni kwamba ‘tutapiga kwenye mshono’. Usiku wa kuamkia jana wakamshusha nchini beki Mkongomani, Hennock Inonga ‘Varane’ ambaye Yanga walishamtumia mpaka tiketi aje Dar.

Kilichotokea ni kwamba Meneja wa beki huyo ambaye wakati akipokea tiketi ya Yanga ghafla akapokea simu ya tajiri mmoja wa Simba na kishika uchumba kikaingia kwenye simu sekunde hiyohiyo na akasisitizwa kwamba; “Tunamtaka huyo mchezaji haraka sana Dar es Salaam.”

Ili kudhibiti zaidi mawasiliano yake na Yanga, akachukua na simu yake akaipiga pini asiwasiliane na yoyote kutoka Tanzania mpaka alipotua nchini akiwa hajui hata anakokwenda kusaini.


 
Yanga walikuwa katika hatua za mwisho kabisa kumleta Inonga na kama sio beki huyo mwenye rasta kuchelewa ndege basi Mwanaspoti linafahamu kwamba angetua sambamba na mshambuliaji, Fiston Mayele ambaye kashasaini Yanga miaka miwili.

Habari zinasema hata cheti za corona alichokuja nacho Simba alilipiwa fedha na Yanga ambao mpaka jana walikuwa hawajui amefikia wapi lakini wanawasiliana na wakala wake ili alipe gharama za tiketi, visa na Corona walizomtumia aje Jangwani akakubali kisha badae akaingia mitini. Inonga kutua Simba ni kama Simba imekumbuka kiporo chake kwani wakati mabingwa hao wakisaka nyota wa kuongeza katika Ligi ya Mabingwa Afrika (Caf) msimu uliopita beki huyo aliwahi kukaribia kusaini kwa wekundu hao lakini ishu ikawa mkwanja lakini vilevile alikuwa anataka kucheza Fainali za Mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).

Simba ilikuwa ikiwinda beki mzoefu na mwenye umri mdogo kwani matarajio yao ni kufanya maajabu kwenye michuano ya kimataifa inayoanza Septemba 11 mwaka huu.


Hatma ya mshambuliaji Meddie Kagere na beki Pascal Wawa iko kwenye hatihati kwani mmoja wao lazima aondoke kupisha nafasi ya Inonga na mwingine anayetua karibuni. Habari zinasema kwamba Kagere huenda akapelekwa kwa mkopo APR ya Rwanda kama itaweza kufikia dau lake la mshahara. Kagere hayupo kwenye mipango ya Didier Gomes licha ya kwamba ni mshkaji wake tokea kitambo sana.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad