Taliban yaichukua Ikulu, Rais akimbia nchi




Wapiganaji wa Taliban wamepiga doria kwenye Mji Mkuu wa Afghanistan, Kabul, leo baada ya vita vilivyodumu kwa miaka 20 nchini humo kufikia mwisho.



Haya yamefanyika wakati maelfu ya watu wamekimbilia katika uwanja wa ndege wa Kabul wakijaribu kukimbia utawala wa kundi hilo wa sheria kali za Kiislamu. Rais Ashraf Ghani aliikimbia nchi hiyo hapo jana wakati wanamgambo hao walipokuwa wameuzingira mji huo mkuu, hiyo ikiwa ndiyo hatua ya mwisho ya ushindi walioupata kwa kuiteka miji yote katika kipindi cha siku kumi tu.

Rais wa zamani wa Afghanistan Hamid Karzai ametoa wito kwa wakaazi wa Kabul kusalia majumbani mwao.”Ndoto yangu ni kuona matatizo ya nchi yetu na mji wetu mkuu yanasuluhusishwa kwa majadiliano. Wapiganaji wa Taliban, popote mlipo, muwalinde watu na maisha yao.

Nawashauri watu wote wasalie majumbani mwao. Tunajaribu kuzungumza na uongozi wa Taliban kutatua matatizo ya watu wa Afghanistan kupitia mazungumzo na udugu, kwa ajili ya taifa letu.”Taliban kwa upande wake limetoa wito kwa Waafghanistan wasiwaogope na kuihakikishia jamii ya kimataifa kuwa hawatolipiza kisasa dhidi ya wale waliunga mkono majeshi yaliyokuwa yakiongozwa na Marekani.

Mamlaka ya viwanja vya ndege nchini Afghanistan ACAA imetangaza kufuta safari za ndege za kibiashara na kusema anga lake litatumiwa na ndege za kijeshi pekee hadi pale kutakapotolewa tangazo jingine.



Kulingana na ACAA, hatua hiyo inalenga kuzuia uporaji na uharibifu na kuonya abiria kutokimbilia uwanja wa ndege. Hata ndege zinazopitia Kabul nazo zimezuiwa.

Muda mfupi uliopita mashuhuda waliarifu kwamba watu watano wamekufa kwenye vuta nikuvute hiyo, huku wanajeshi wa Marekani wakiwa wameimarisha ulinzi wakati wakiwahamisha watumishi hao wa ubalozi. Haijajulikana iwapo waliuawa kwa risasi ama mkanyagano baada ya mashuhuda hao kusema mwanajeshi mmoja wa Marekani alifyatua risasi hewani ili kuwazuia abiria waliokuwa wakijaribu kulazimisha kuingia kwenye ndege.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad