Dar/Dodoma. Wakati Spika wa Bunge, Job Ndugai, akisema kodi ya miamala ya simu inapaswa kutazamwa upya ili kuwapa unafuu wananchi, Serikali imesema imekusanya zaidi ya Sh48.4 bilioni katika mwezi mmoja wa utekelezaji ukusanyaji wa tozo hiyo.
Akitoa taarifa kwa umma jijini Dar es Salaam juzi, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, alisema fedha hizo zimepelekwa kwenye miradi ya afya, elimu na miundombinu ya barabara.
Katika kiasi hicho kilichokusanywa kuanzia Julai 15, Dk Mwigulu alisema Sh22.5 bilioni zimepelekwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (Tamisemi) kwa ajili ya kujenga vituo vya afya 90, huku Sh15 bilioni zikitarajiwa kupelekwa ndani ya mwezi huu kujenga vituo vingine 60 ili kufikisha vituo 150 nchi nzima.
“Watanzania wameendelea kufanya miamala kama kawaida; walipaza sauti juu ya mambo ambayo yanapaswa kuwekwa sawa. Katika wiki nne za mwanzo jumla ya miamala milioni 9.9 ilifanyika, haina tofauti sana na siku za nyuma ambapo ilikuwa kati ya milioni 10 na 11. Tofauti sio kubwa,” alisema Dk Mwigulu huku akisita kueleza mlinganisho wa thamani ya miamala katika kipindi hicho na kilichopita.
Aidha, alisema malengo ya Serikali ni kupata fedha za kuhudumia wananchi kwani itakuwa ni aibu wanafunzi kuendelea kusomea chini ya mti au kujengewa vyoo vya shule kwa kutegemea wahisani.
Kuhusu tozo mpya ya mafuta iliyoanzishwa Dk Mwigulu alisema kwa wiki mbili za mwazo Serikali ilikusanya Sh24 bilioni na mpaka jana makusanyo yalikuwa zaidi ya Sh48 bilioni.
“Julai zilipatikana Sh24 bilioni ambazo ni mahsusi kwa ajili ya ujenzi wa barabara zisizopitika. Tangu umeanza mwezi huu, tutakuwa na bilioni nyingine zaidi ya 20 ambazo ukijumlisha utapata zaidi ya Sh48 bilioni,” alisema Dk Mwigulu.
Mchumi na mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Delphin Rwegasira alisema ni mapema kuzungumzia tija na ufanisi wa fedha zilizopatikana na namna zitakavyotumika.
“Sishangai kwa wiki hizo nne makusanyo kuwa Sh48 bilioni, ni lazima zingepatikana sababu ni makato ya moja kwa moja ya miamala ya simu. Tunasubiri Bunge na waziri kutupa majibu,” alisema.
Spika aungana na wananchi
Licha ya msimamo tofauti aliokuwa nao awali, Ndugai alikiri kuwa tozo ya miamala ya simu, licha ya uzuri wa dhamira yake, inawaumiza wananchi hivyo inapaswa kuangaliwa.
Hii ni mara ya kwanza kwa Ndugai kukiri hadharani kuhusu kilio cha miamala hiyo, kwani amekuwa akiipigia chapuo kwamba lazima watu walipe kodi iliyopitishwa na Bunge.
Akizungumza katika kongamano la Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kundi la wenye ulemavu lililofanyika juzi, Ndugai ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Kongwa, alisema ipo haja suala hilo likarudishwa bungeni ili liwekwe sawa kutokana na kelele zinazopigwa na wananchi.
“Sisi wawakilishi wenu tulipitisha kwa nia njema, lakini labda kuna maeneo hayakuangaliwa vizuri. Basi tutajaribu kutimiza vizuri huko tunakokwenda kama Rais Samia alivyoelekeza. Lakini kodi hii ni muhimu sana kwa ajili ya maendeleo ya Taifa,” alisema Ndugai.
Katika maboresho anayoyatarajia, Spika alisema anadhani ni vyema mtumaji ndiye alipe, lakini anayetumiwa asilipe kama ilivyo sasa ambapo pande zote wanatakiwa kulipa.
Mawaziri wafunguka
Katika mkutano wake, Dk Mwigulu aliambatana na Waziri wa Tamisemi, Ummy Mwalimu, Waziri wa Mawasiliano na Teknolijia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Juma Malik Akil.
Waziri Ndugulile alisema kikosi kazi kilichopewa jukumu la kuzipitia upya gharama za tozo hizo, kitatoa majibu ndani ya mda mfupi na kuwaomba Watanzania kuendelea kuwa na subira.
Kwa upande wake, Waziri Ummy alisema wizara yake imepokea Sh22.5 bilioni kujenga vituo vya afya katika halmashauri 82.
“Fedha hizi tayari zipo kwenye akaunti za halmashauri husika, zitajenga vituo vya afya katika tarafa ambazo hazina vituo vya afya...” alisema Ummy.
Waziri huyo pia alisema Sh15 bilioni zinatarajiwa kuwasili Jumatatu ijayo kwa ajili ya ujenzi kwa kupitia utaratibu wa kuwashirikisha wananchi na kuzitaka halmashauri husika kuwatumia makandarasi wa ndani.
Waziri Ummy pia alisema mwakani vitahitajika vyumba 10,447 vya madarasa kwa ajili ya kuchukua wanafunzi wa kidato cha kwanza, ambao idadi yao inatarajiwa kuongezeka mara mbili.
“Kutokana na sera ya elimu bure, tunatarajia watakaofaulu darasa la saba kwenda kidato cha kwanza mwakani watakuwa 944,855 kutoka 422,403 sawa ongezeko la wanafunzi 522,452 hivyo kuhitaji madarasa mapya 10,447,” alisema.
Aliongeza kuwa Agosti 23 Tamisemi itapokea Sh7 bilioni zitakazotumika kukamilisha ujenzi wa vyumba 560 vya madarasa ya shule za msingi na sekondari.
Sintofahamu kodi ya majengo
Baada ya tangazo la TRA kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kueleza kuanza kukusanya kodi hiyo kwa kila anunuaye umeme, kumekuwa na maoni tofauti kutoka kwa wananchi baadhi wakisema utaratibu huo hauna uhalisia kwa sababu watu wengi wanaishi kwenye nyumba za kupanga.
“Tunaomba Serikali ilitazame hili suala kwa sababu sisi wapangaji tutakuwa tunalipia nyumba ambazo si zetu. Kwa nini nilipe mimi wakati mwenye nyumba yupo na anaweza kulipa mwenyewe?” alihoji Stephen Wando, mkazi wa Tabata.
Mchumi mwandamizi na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alisema kuwatoza wapangaji kodi ya jengo ni kuwanyima haki kwa sababu anayepaswa kulipa ni mmiliki.
“Kilichoangaliwa ni urahisi wa kulipa. Ni muhimu kutazama uhalali wa jambo lenyewe unalohitaji kulifanya,” alisema.
Wakati huohuo, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), limesema linawasiliana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuona jinsi ya kutekeleza ukusanyaji wa kodi ya majengo kupitia mfumo wa Luku kwa kuwatambua wapangaji waliolipa na kiasi walicholipa, ili kuweka utaratibu wa namna ya kuchukua jukumu hilo.