KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu nchini Tanzania (LHRC), kimefungua kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, kupinga tozo za miamala ya simu, zilizoanza kutumika tarehe 15 Julai 2021. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Taarifa hiyo imetolewa leo Ijumaa, tarehe 6 Agosti 2021 na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga.
Katika kesi hiyo, LHRC inapinga tozo hiyo kwa madai kwamba ni mzigo kwa wananchi, hasa wasio na uwezo wa kifedha.
“LHRC kimefungua kesi hiyo kufuatia kupitishwa kwa mapendekezo ya Bajeti ya Serikali 2021/22, pamoja na sheria ya fedha iliyopelekea kuweka tozo katika miamala ya fedha, inayofanywa kwa njia ya simu. Jambo ambalo limeongeza mzigo kwa mwananchi wa kawaida, pamoja na wafanyabiashara wadogo na wakubwa,” amesema Henga.
Mkurugenzi huyo wa LHRC amesema, wanaiomba mahakama hiyo ipitie Sheria ya Mfumo wa Malipo ya Kitaifa Sura. 437, pamoja na kanuni zake zilizoweka tozo hiyo, ili iamuru Serikali kuiondoa au kupunguza viwango vinavyotozwa kupitia tozo hiyo.
“Katika kesi hii tunaomba viwango vipunguzwe kama itakuwa lazima iwepo au iondolewe. Kwa sababu tunaona mzigo zaidi kwa wananchi ambao wanalipa kodi na wanapokuwa wanatoa pesa wanakatwa kodi na tozo kwa kiasi fulani,” amesema Henga.
Henga amesema kesi hiyo ilifunguliwa tarehe 27 Julai 2021 na ilisikilizwa kwa mara ya kwanza, tarehe 5 Agosti 2021 mbele ya Jaji John Mgeta.
“LHRC kilifungua shauri la namba 11 ya mwaka 2021, kuomba mapitio ya Mahakama Kuu (Judicial Review), kuhusu National Payments System Act Cap. 437, pamoja na kanuni zake zilizoweka tozo katika miamala ya fedha kwa njia ya simu,” amesema Henga.
Henga amesema, kesi hiyo itasikilizwa tena mahakamani hapo kwa mara ya pili, tarehe 16 Agosti 2021.
Tangu tozo hiyo ianze kutumika, makundi mbalimbali yaliipinga kwa maelezo kwamba ni mzigo kwa wananchi na kuiomba Serikali iiondoe au ipunguze viwango vyake.
Tarehe 27 Julai 2021, akiwaapisha mabalozi Ikulu, jijini Dar es Salaam, Rais Samia Suluhu Hassan, alisema Serikali yake inayafanyia kazi malalamiko hayo kuhusu tozo hiyo.
Rais Samia alisema Serikali yake haitaiondoa tozo hiyo, bali itaangalia namna bora itakayowezesha wananchi kuilipa bila maumivu.