Ukweli kuhusu chanjo corona nguvu za kiume



 
WATAALAMU wa afya nchini wamebainisha hakuna uhusiano kati ya chanjo na kuongeza nguvu za kiume.

Mkurugenzi wa Kuratibu Utafiti wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk. Paul Kazyoba.
Mkurugenzi wa Kuratibu Utafiti wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk. Paul Kazyoba, aliyasema hayo jijini Dar es Salaam juzi alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu chanjo ya UVIKO-19.

Alisema hakuna utafiti uliofanywa kuhusu uhusiano wa chanjo ya Johnson & Johnson inayotolewa nchini na kuongeza au kupunguza nguvu za kiume.

“Licha ya kuwa hakuna utafiti uliofanywa kwetu sisi wanaume tuliochanja, mimi binafsi sikuona mabadiliko yoyote kuhusu nguvu za kiume kama ni hasi au chanya, kwa maana hiyo ninaweza kusema chanjo hii haina uhusiano na suala hili,” alisema Dk. Kazyoba.

POMBE MARUFUKU

Kuhusu unywaji wa pombe, Dk. Kazyoba, alisema inashauriwa kuwa anayetaka kuchanja, anapaswa kutokunywa pombe siku tatu kabla na baada ya kuchanja.


 
“Ni ngumu ‘kum-control’ (kumdhibiti) mtu mmoja mmoja asinywe pombe lakini ni muhimu wakazingatia hili hasa ikizingatiwa kuwa chanjo haifanyi kazi kwenye mwili wa binadamu mara tu baada ya kuchanja,” alisema.

Dk. Kazyoba alisema mgonjwa anayekiuka masharti na kunywa pombe kabla na baada ya kuchomwa chanjo, yupo katika hatari ya kupata madhara kwenye ini.

Alisema kuwa madhara yatajitokeza kwenye ini kwa sababu lina kazi ya kuchuja sumu katika mwili, hivyo litalazimika kuanza kupambana na sumu ya pombe wakati huo huo kupokea chanjo inayoingia mwilini.


Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani na Mbobezi wa Moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Tatizo Sanga, alisema chanjo huanza kufanya kazi kwenye mwili wa mtu kuanzia siku saba hadi 15.

Alisema baada ya mtu kuchoma chanjo, mwili huanza kujipanga kutengeneza utaratibu wa kuipokea kabla ya kuanza kufanya kazi ndani ya wiki mbili.

MAGONJWA SUGU

Kuhusu watu wenye magonjwa sugu kupata chanjo, Dk. Sanga alisema ni muhimu kundi hilo kupewa chanjo ili kuwaepusha na mashambulizi ya UVIKO-19 yanayoweza kuwaweka katika hatari tofauti na wasio na magonjwa hayo.

“Watu wenye matatizo ya moyo ni muhimu kupata chanjo ili waepuke changamoto ya upumuaji inayoongeza shambulizi kwenye mwili na kuleta uwezekano wa mgonjwa kupoteza maisha,” alifafanua Dk. Sanga.


 
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani na Mbobezi wa Mapafu na Mahututi, Pauline Chale, alisema wagonjwa wenye maambukizi ya UVIKO-19 hupata madhara kwenye mapafu.

Alisema kuna milango ipo kwenye mapafu, moyo, ini na mfumo wa tumbo ambayo UVIKO-19 huitumia kujishikiza hadi kufika kwenye seli za damu.

Alisema kutokana na mwingiliano huo wa kirusi, mgonjwa hupanwa mapafu na kushindwa kuvuta hewa na ndio sababu ya kumwekea hewa ya Oksijeni ambayo hutumia hadi wiki nne ili kurejea katika hali ya kawaida.

“Kutokana na kuwa mgonjwa anakaa kwenye Oksijeni kwa wiki mbili hadi nne kama hatapoteza maisha, hutumia mitungi mitatu hadi mitano kwa siku, wakati gharama ya kumlaza mgonjwa mmoja kwa siku ni Sh. 500,000, hivyo utaona gharama zilivyo kubwa,” alisema.


Dk. Pauline aliwataka wananchi kuendelea kujikinga na kupata chanjo kwa manufaa yao binafsi na vizazi vyao.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad