Umoja Wa Afrika Kuipatia Tanzania Chanjo Milioni 17 Za Corona




Umoja wa Afrika umeitengea Tanzania dozi milioni 17 za chanjo za UVIKO- 19 kupitia mpango wa Umoja huo wa kuzisaidia Nchi wanachama kupata chanjo kwa ajili ya Wananchi wake.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula ameyasema hayo Addis Ababa Nchini Ethiopia alipokutana kwa mazungumzo na Jumuiya ya Watanzania waishio Nchini Ethiopia (Diaspora) waliotaka kufahamu hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kupambana na UVIKO -19 ikiwa ni pamoja na suala la chanjo.

Aidha Balozi Mulamula amewataka Watanzania wanaofanya kazi katika Mashirika na Taasisi mbalimbali za Kimataifa kusaidia upatikanaji dozi nyingine za chanjo ya UVIKO 19 ili kuwawezesha Watanzania wengi  kupata chanjo hiyo kutokana na  mwamko wa Watanzania kuongezeka mara  baada ya kuzinduliwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika tukio jingine Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Ethiopia Mhe Sahle – Work Zewde Addis Ababa nchini Ethiopia ambapo Tanzania na Ethiopia zimekubalina kuendelea kutumia ndege za shirika la Ethiopia kutangaza vivutio na kusafirisha Watalii kutoka mataifa mbalimbali kuja Tanzania.

Aidha Balozi Mulamula amemhakikishia Rais Sahle – Work Zewde kuwa Tanzania itaendelea kutekeleza maeneo yote ya ushirikiano ambayo Rais Zewde alikubaliana na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa ziara ya Rais huyo Chato nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na suala la kuwarejesha Nchini Ethiopia wahamiaji wanaoshikiliwa katika magereza mbalimbali.

Kwa upande wake Rais wa Ethiopia  Mhe. Sahle – Work Zewde amesisitiza kuendelea kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Nchi hiyo hususani katika kutatua changamoto zinazozuia maendeleo miongoni mwa Mataifa hayo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad