Dar es Salaam. Wakati Rais Samia Suluhu Hassan akifanya uteuzi wa wakurugenzi watendaji wa halmashauri za majiji, manispaa, miji na wilaya, uteuzi wa wakurugenzi wawili umeibua gumzo mitandaoni baada ya kuteuliwa kwenye halmashauri mbili tofauti kila mmoja.
Katika taarifa iliyotolewa leo Agosti 2, 2021 na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais - Ikulu, Dollar Kusenge ameteuliwa kuwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri za Kasulu na Njombe wakati Lutengano Mwaliba akiteuliwa kuwa mkurugenzi wa halmashauri za Bukombe na Misungwi.
Alipotafutwa kufafanua uteuzi huo, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais – Ikulu, Jaffar Haniu hakupatika kwenye simu yake.
Kusenge naye alipoulizwa kama amepata maelezo ya uteuzi wake, amesema suala hilo liulizwe kwa mamlaka husika.
“Mimi nafikiri hilo mnaweza kuuliza mamlaka husika,” amesema Kusenge ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa mwenyekiti wa chama cha Msalaba Mwekundu mkoa wa Dar es Salaam.
Hata hivyo, baadhi ya watu wanafikiri kuna makosa ya kiuandishi katika taarifa hiyo kwa sababu ni vigumu kwa mkurugenzi kusimamia kwa ukaribu halmashauri mbili tofauti ambazo ziko mbali kijiografia.
“Hawa wanaoandaa hizi taarifa wakati mwingine wanakosea, tumeshudia taarifa nyingi zikiwa na makosa, kwa mfano, ile orodha ya majina ya walimu wapya, jina moja lilijirudia mara nyingi,” amesema mkazi wa Tabata, Alex Chiduo.
Boniface Nyamarege ameandika katika mtandao wa Facebook kwamba: “Katibu Mkuu huyu sijui anatupeleka wapi...hivi huwa hawapitii taarifa baada ya kuiandaa ama Bora liende...”