Hali inayojiri Afghanistan baada ya Taliban kuchukuwa udhibiti inawafanya viongozi wa mataifa jirani na jumuiya za kikanda kutafakari hatua wanazopaswa kuzichukua, kuepusha kusambaa kwa mzozo huo hadi katika nchi zao.
Afghanistan ilikuwa agenda kuu ya mazungumzo ya simu baina ya rais wa Marekani Joe Biden na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel Jumatano jioni.
Ofisi ya Kansela Merkel imesema viongozi hao wawili wametilia mkazo ulazima wa kuwawezesha Waafghanistan waliofanya kazi na Ujerumani, wengi iwezekanavyo, kuweza kuondoka nchini mwao na kwenda mahali salama.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Heiko Maas amesema balozi wa Ujerumani mjini Kabul amewasiliana na viongozi wa Taliban walioko mjini Doha, Qatar akiwataka kuwaruhusu raia hao wa Afghanistan kufika katika uwanja wa ndege.
Duru za hivi punde zimesema Marekani imepata taarifa kuwa Wataliban walikuwa wakiwazuia raia wa Afghanistan kufika katika uwanja wa ndege wa Kabul.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Joe Biden wa Marekani wamezungumza kuhusu namna ya kuwasaidia raia wa Afghanistan kutorokea mahali salama
Maas amesema tangu Jumapili, ndege za Ujerumani zimeweza kuwasafirisha watu wapatao 500 nje ya Afghanistan, takriban 200 miongoni mwao wakiwa Waafghanistan. Amesema Ujerumani inayo nia ya kuendelea kuwahamisha watu wengi kiasi hicho mnamo siku zijazo, akiongeza kuwa anaamini muda wa kufanya safari kama hizo ni mfinyu.
Wanajeshi wa Marekani waweza kubaki Afghanistan baada ya Agosti 31
Nchini Marekani, Rais Joe Biden amefanya mahojiano na kituo cha televisheni cha ABC, na kusema anaweza kubakisha wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan hata baada ya tarehe ya mwisho ya Agosti 31, ikiwa kutakuwepo raia wa Marekani ambao wanasalia huko. Inaaminika kuwa hadi sasa wapo Wamarekani wapatao 15,000 wanaosubiri kuondolewa Afghanistan.
Kwingineko, Slovenia ambayo inashikilia urais wa Umoja wa Ulaya ambao ni wa kupokezana kila baada ya miezi sita, imeitisha mkutano wa dharura kujadili njia za kuzuia mzozo wa wakimbizi wa Afghanistan barani Ulaya. Waziri wa mambo ya ndani wa nchi hiyo, Ales Hojs amewaambia waandishi wa habari kuwa mkutano huo unaweza kufanyika katika muda wa siku chache zijazo.
Ndege kama hii ya jeshi la Ujerumani ni miongoni mwa zinazotumika kuwasafirisha maelfu ya watu kutoka mjini Kabul
Sio Umoja wa Ulaya tu unaojishughulisha na sintofahamu inayoendelea Afghanistan. Rais wa Iran, Ebrahim Raisi amefanya mazungumzo na rais wa China Xi Jinping na pia rais Vladimir Putin wa Urusi, na kwa mujibu wa tangazo la Ikulu ya mjini Tehran, viongozi hao watatu wamekubaliana kushirikiana kwa ajili ya amani na utulivu nchini Afghanistan.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika kwa njia ya simu, Marais Xi, Putin na Rais wamehimiza makundi yote nchini Afghanistan kuja pamoja, na kutumia kuondoka kwa vikosi vya Marekani na washirika wake kama fursa ya kujenga amani ya kudumu nchini mwao.
Ndani ya Afghanistan kwenyewe, kitendo cha Wataliban kutumia mabavu kuzima uasi wa watu katika mji wa Jalalabad kimesababisha wimbi la hofu juu ya uwezo wa kundi hilo la itikadi kali ya kiislamu lisilo na taasisi zinazoeleweka, kuitawala nchi kwa amani kama walivyoahidi. Kundi la watu liliandamana, na kuzing'oa bendera za Taliban huku wakipeperusha ile ya Afghanistan. Inaarifiwa kuwa Wataliban waliuwa watu wasiopungua watatu katika purukushani hizo.
Katika taarifa nyingine, Wataliban wamefanya mazungumzo na rais wa zamani wa Afghanistan Hamid Karzai na aliyekuwa afisa mwandamizi katika utawala ulioangushwa, Abdullah Abdullah, juu ya namna ya kuunda serikali.
Rais Ashraf Ghani aliyeipa kisogo Afghanistan na kukimbilia katika Umoja wa Falme za Kiarabu, amesema anaunga mkono mazungumzo hayo yaliyofanyika mjini Kabul.