Wafanyabiashara wawili wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu wakikabiliwa na Mashtaka matatu ikiwemo la kuchapisha maudhui ya uongo dhidi ya Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa.
Washitakiwa hao ni Adam Thabiti na Heri Said wote wakiwa wakazi wa Dar es Salaam ambapo wamefikishwa Mahakamani hapo na kusomewa Mashtaka yao na wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga mbele ya hakimu mkazi mkuu wa mahakama hiyo Evodia Kyaruzi.
Katika shitaka la kwanza washitakiwa hao wanadaiwa kutenda mnakosa hayo mnamo Juni 20,2021 kwa kusambaza messeji za uongo kwamba Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametumbuliwa wakati wakijua sio kweli.
Katika shitaka la pili wakili Katuge amedai washitakiwa hao wanadaiwa kuchapisha maudhui ya uongo dhidi ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kupitia You tube Channel yao inayoitwa Bongo News kosa ambalo wanadaiwa kulitenda Januari 2,2021.
Aidha katika shitaka la tatu washitakiwa hao wanadaiwa kuendesha Online channel bila kuwa na kibali cha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA.
Washitakiwa wamekana kutenda makosa hayo ambapo wameomba mahakama kuwapa dhamana kwa kuwa walipewa dhamana wakiwa chini ya Polisi huku upande wa Mashtaka ukiwasilisha hoja ya kuomba mahakama isitoe dhamana kwa ajili Usalama wao dhidi ya baadhi ya wananchi wenye hasira kali.
Hakimu Evodia ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 20,2021 na washitakiwa wamerudishwa rumande.