Jumla ya watu 12 wameuawa karibu na uwanja wa ndege wa Kabul tangu Jumapili, kulingana na afisa wa Taliban.
Afisa huyo, ambaye alizungumza na shirika la habari la Reuters bila kutaja jina, alisema vifo hivyo vilisababishwa na risasi au kukanyagana.
Aliwahimiza umati kwenye malango waende nyumbani ikiwa hawana haki ya kusafiri na akasema Taliban "hawataki kumuumiza" yeyote katika uwanja wa ndege.
Kumekuwa na matukio ya vurugu yaliyoripotiwa wakati maelfu wakijaribu kuondoka nchini humo.
Uwanja wa ndege wa Kabul unabaki chini ya udhibiti wa Marekani lakini barabara zinazozunguka zinalindwa na Taliban.
Mashahidi wameripoti wataliban wenye silaha wamekuwa wakizuia watu, pamoja na wale walio na hati, kuingia ndani ya kiwanja hicho.