Watu 47 walipoteza maisha na angalau wengine 19 walijeruhiwa kwenye shambulizi la msafara wa raia na vikosi vya usalama katika mkoa wa Sahel nchini Burkina Faso.
Msafara uliokuwa umebeba wanajeshi na wafanyakazi wa kujitolea wa ulinzi wa raia ulishambuliwa na magaidi katika wilaya ya Gorgadji mkoani Soum.
Katika shambulizi hilo, raia 30, maafisa 14 wa vikosi vya usalama na wafanyakazi 3 wa kujitolea waliosaidia vikosi vya usalama walipoteza maisha.
Baada ya shambulizi hilo, ambalo watu wasiopungua 19 pia walijeruhiwa, iliripotiwa kuwa vikosi vya usalama viliwaangamiza magaidi 58.
Vikundi vya kigaidi vinavyohusiana na Al-Qaeda na Daesh vinavyofanya kazi katika nchi jirani ya Mali vimekuwa vikitekeleza mashambulizi mara kwa mara kaskazini na mashariki mwa Burkina Faso tangu mwaka 2015.
Ijapokuwa Burkina Faso inafanya operesheni za pamoja za kijeshi na jirani yake mwingine wa Sahel, Niger, imeshindwa kudhoofisha nguvu za vikundi vya kigaidi vilivyoko Mali.
Kulingana na data ya Umoja wa Mataifa, watu 17,500 wamelazimika kuondoka nchini kwa sababu za usalama tangu mwanzo wa mwaka.