Akizungumzia kuhusu ugonjwa wa UVIKO 19, Waziri Mkuu amewataka wananchi wafuate maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya katika kujinga na ugonjwa huo na pale wanapoona dalili ambazo hawazielewi wawahi katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa uchunguzi na matibabu.
“Kama mnavyofahamu, kuwa dunia nzima ipo kwenye wimbi la tatu la UVIKO 19. Janga hili lipo nchini na limesababisha baadhi ya ndugu zetu kupoteza maisha na wengine kuendelea kuugua. Kwa msingi huo ni muhimu kwetu kuendelea kuchukua tahadhari kwa kujikinga na maambukizi ya UVIKO 19.”- Waziri Mkuu
Amesema kuwa chanjo ya UVIKO 19 inapatikana na inasambazwa nchini kote ikiwemo hapa Dodoma ambapo huduma hiyo inatolewa katika vituo 89 ndani ya mkoa.
“Sambamba na vituo hivi, pia ipo huduma ya mkoba (mobile) ambapo watumishi wa afya wanakwenda katika maeneo yenye watu wengi ikiwemo makampuni ya ujenzi na kutoa huduma”- Waziri Mkuu