WAKATI jana Jumamosi ilitarajiwa kuwa Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi ya Michezo (CAS) kutoa majibu ya kesi kati ya Klabu ya Yanga na mchezaji, Bernard Morrison raia wa Ghana, Mkurugenzi wa Sheria na Wanachama wa klabu hiyo, Patrick Simon amezitaja gharama walizotumia hadi kesi hiyo inakamilika.
Patrick alisema mchakato huo wa kesi ya kimkataba kati ya Morrison na Yanga inaanza hadi inamalizika, wametumia shilingi milioni 98, ikiwa ni malipo ya ada mbalimbali huko CAS.
Akizungumzia mchakato huo, Patrick alisema wao waliona kuna haja ya kuipigania haki yao huko CAS na ndiyo maana walikuwa tayari kutumia gharama kubwa ili kuitafuta haki hiyo.
“Mpaka kesi yetu inamalizika tumetumia milioni 98 kwenye kulipia ada mbalimbali kule CAS za kuendesha kesi hii. Kwa hapa Tanzania nafikiri sisi ndiyo timu ya kupeleka kesi huko.“
Tuliamua kufanya hivyo kwa sababu tuliona kuwa sehemu hatutendewi haki, watu walikuwa wanasikia tu kuna kitu kinaitwa CAS na walidhani hatutafanikiwa, lakini hatimaye kila mtu amejua nini tulikuwa tunahitaji,” alisema Patrick.
Yanga inadai kwamba, Morrison ni mchezaji wao mwenye mkataba hadi 2022 kutokana na kusaini miaka miwili baada ya ule wa awali wa miezi sita kumalizika Julai 2020.Kwa upande wa Morrison, anasema hana mkataba mwingine na Yanga baada ya ule wa miezi sita kumalizika, jambo lililomfanya kuwa huru kutua Simba alipo sasa.