Dar es Salaam. Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amebainisha kuwa ikitokea akateuliwana Rais Samia Suluhu Hassan kuhudumu serikalini hatokubali kwa sababu nguvu na maono yake kwa sasa ni kujenga chama kwanza.
Zitto amesema hayo alipohojiwa na kituo cha televisheni cha Star Tv Jumamosi usiku na kuulizwa tafanyaje ikiwa Rais Samia atamteua na kumpa nafasi kutumika serikalini.
Akijibu swali hilo, Zitto alisema “nataka nijenge chama, huwezi kujenga Taifa ukiwa na vyama goigoi, lazima uimarishe vyama vya siasa ili uwe na vyama madhubuti, vizae Serikali madhubuti, kwa sasa hivi naona utume wangu sio kuwa serikalini bali kuijenga ACT kiwe chama imara kinachoweza kudhibiti mapigo ya aina yoyote na kujenga Serikali itayohudumia Watanzania vizuri. Nitamshukuru Rais kwa imani yake kwangu ila nitamuomba atafuta mtu mwingine kuifanya kazi ambayo mimi ningeifanya ili mimi nipate nafasi ya kukijenga ACT Wazalendo.”
Akizungumzia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ambao ripoti yake ilipokelewa Jumamosi na Rais Samia kutoka Tume ya Uchaguzi, Zitto alisema hakukuwa na uchaguzi bali operesheni ya kuirudisha Tanzania kwenye mfumo wa chama kimoja.
“Binafsi sikushindwa uchaguzi wowote halali Kigoma, nimefanya kazi kubwa sana Kigoma kipindi chote nilichokuwa kwenye siasa na nimapandisha hadhi ya Mkoa wa Kigoma, uchaguzi ulikuwa mbovu, sio kwamba wana Kigoma walinikataa,” alisema Zitto.
ACT Wazalendo pamoja na NCCR-Mageuzi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kiligoma kuhudhuria makabidhiano ya ripoti ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana hivyo Rais akapokea ripoti hiyo mbele ya wawakilishi wa vyama vingine.
Kuhusu tofauti ya utawala wa Rais Samia na uliopita, Zitto alisema kuna baadhi ya mambo Rais Samia amebadilisha akatolea mfano uhuru wa vyombo vya habari lakini yapo yaliyotarajiwa kubadilika ila bado yapo.
“Kwa mfano kukamatwa kwa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, wanachama wa Chadema Mwanza na mmoja wa kiongozi wetu, mpaka sasa siamini kama kulikua na sababu ya kumkamata Mbowe na kumweka ndani mpaka sasa,” alisema.
Zitto alisema kuna umuhimu kwa vyama vya siasa kukutana na Rais Samia kujadili namna ya kufanya siasa nchini.