CHAMA cha ACT-Wazalendo kimesema hakitashiriki kikao kilichopangwa kuvikutanisha vyama vya siasa na Jeshi la Polisi Oktoba 21, mwaka huu.
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi:PICHA NA MTANDAO
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwenye vyombo vya habari jana na Katibu wa Habari, Uenezi, Uhusiano na Umma wa chama hicho, Salim Bimani, wamefikia uamuzi huo baada ya kutafakari kwa kina.
“Tumepata taarifa kupitia vyombo vya habari kuwa kikao cha Jeshi la Polisi na vyama vya siasa kilichoitishwa na Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa kimepangwa kufanyika Oktoba 21, mwaka huu. Baada ya kutafakari kwa kina, ACT-Wazalendo tumeamua kuwa hatutashiriki kikao hicho,” alisema Bimani.
Alisema sababu za chama hicho kuamua kutoshiriki kikao hicho ni pamoja na ratiba ya kikao baina ya vyama hivyo na Jeshi la Polisi kuingiliana na ratiba na vikao vya viongozi wakuu wa chama hicho.
“Oktoba 21 hadi 22, mwaka huu, viongozi wakuu wa chama chetu watakuwa kwenye mkutano mkuu wa kitaifa wa haki, amani na maridhiano ulioitishwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania(TCD). Mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan,” alisema Bimani.
Alisema sababu nyingine iliyochangia chama hicho kufikia uamuzi huo ni kutopatiwa mrejesho wa barua yao waliyoituma kwa Msajili wa vyama ya kuomba kikao hicho kimshirikishe Waziri wa Mambo ya Ndani.
“Baada ya msajili wa vyama vya siasa nchini kutangaza kikao na vyama hivyo, ACT-Wazalendo kupitia kwa Kiongozi wa chama Zitto Kabwe, kilimwandikia barua kuwa kikao hicho kimjumuishe Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye ndiye mwenye dhamana ya kisiasa na Jeshi la Polisi. Hadi sasa hatujapata mrejesho wa suala hilo na mwelekeo ni kuwa kikao hicho kitakuwa cha polisi na vyama vya siasa pekee,” alisema Bimani.
Pia chama hicho kinadai kwamba sababu nyingine ya kuamua kutoshiriki kikao hicho ni kutokana na matamshi ambayo kimekuwa kikiyasikia kwa baadhi ya viongozi wanaotarajiwa kukutana nao, kuonyesha kwamba huenda kikao hicho kikatumika kubinya zaidi shughuli za kisiasa nchini.
“Matamshi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro, baada ya kikao chake na Msajili wa Vyama vya Siasa hayaonyeshi nia njema ya kikao hicho,” alisema Bimani.
“Kauli yake kuwa nchini Tanzania hakuna shida kuhusu mikutano ya nje na kwamba tatizo lipo kwenye mikutano ya ndani na inabidi sheria iwekwe sawa, ni dalili ya wazi kuwa kikao hicho kinaweza kutumika kubinya zaidi shughuli za kisiasa nchini.”
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, alitangaza kufanyika kwa vikao hivyo vikiwa na lengo la kumaliza misuguano ambayo imekuwa ikijitokeza baina ya Jeshi la Polisi na vyama hivyo na tayari kikao cha awali kimefanyika kati ya ofisi ya Msajili na Jeshi hilo na Oktoba 21 itakuwa ni zamu ya vyama hivyo la Jeshi la Polisi.