Kijana wa miaka 19 mkazi wa Bukoba, aliyezaliwa na jinsi ya kike na baadaye kuota sehemu za siri za kiume zilizopelekea sehemu za kike kuzibwa, anaomba msaada wa fedha aende nje ya nchi kuongezwa ukubwa wa maumbile ya kiume, yatakayomwezesha kufanya tendo la ndoa na kuzaa watoto.
Kijana anayeomba msaada
Kijana huyo ambaye jina lake limehifadhiwa kwa sasa anavaa mavazi ya kiume na kutumia majina ya kiume aliyoyapata baada ya kula kiapo mahakamani baada ya kukana majina yake ya kike aliyopewa awali mara baada ya kuzaliwa, majina ambayo aliyatumia kuanzia darasa la kwanza hadi la saba, na kusema anatamani kuoa na kupata watoto.
"Nilipomaliza darasa la saba nilichaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari, lakini kwa kuwa nilishabadilika na kuwa wa kiume, niliomba shuleni niruhusiwe nivae sare za kiume lakini walikataa ikabidi niache shule," amesema kijana huyo
Mama mzazi wa kijana huyo Geneveva Gaspale, amesema kuwa mtoto wake alimzaa akiwa na jinsia ya kike ila kadiri alivyokuwa akikua alibadilika na kuota sehemu za siri za kiume na kudai kwamba pia wadogo zake wawili ambao wana jinsi za kike wameanza kubadilika kama ilivyotokea kwa ndugu yao.
Mama huyo amesema baada ya mtoto huyo kuota sehemu za siri za kiume alizibwa sehemu ya kwanza ya kike katika hospitali ya Taifa Muhimbili, lakini changamoto imebaki kuwa jinsia ya kiume iliyobaki ni ndogo, na wanahofia kuwa haiwezi kufanya kazi.