Askofu Gwajima ajibu mapigo ya kamati ya Bunge




Askofu Josephat Gwajima
MBUNGE wa Kawe mkoani Dar es Salaam (CCM), Askofu Josephat Gwajima, amewaeleza waumini wake wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, kwamba yeye sio mtu mbaya kama alivyotuhumiwa na Kamati ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Askofu Gwajima ametoa kauli hiyo leo Jumapili wakati akihubiri katika kanisani hilo lililopo Ubungo, mkoani Dar es Salaam, siku tano baada ya tarehe 31 Agosti 2021, Bunge kumpa adhabu ya kutohudhuria mikutano yake miwili mfululizo.

Bunge lilitoa adhabu hiyo, baada ya kamati yake ya maadili kumtia hatiani Askofu Gwajima, katika kosa la kulidhalilisha na kulichonganisha na Serikali pamoja na wananchi, kufuatia kauli zake alizotoa akipinga mpango wa utoaji chanjo ya Ugonjwa wa Korona (UVIKO-19), kwa wananchi.

“Kama mlivyosikia niliitwa na kamati ya madili na nilipotoka kwenye hiyo kamati wengi mliniuliza kimejiri nini, nikasema sitasema chochote mpaka kamati izungumze kwanza, sababu imezungumza ngoja na mimi nizungumze,” amesema Askofu Gwajima.


 

Amesema “kamati ilipozunugumza walinionesha ni mtu mbaya sana, basi halitakiwi hata kuwa Askofu wa Kanisa. Unajua unapomuongelea kiongozi wa kanisa kwa namna ambavyo unatengeneza uharibifu kwa kanisa, hakuna kiongozi wa kiroho anaweza kuvumilia kwa maneno hayo.”

Askofu Gwajima amedai kuwa, alituhumiwa kuwa mkorofi kutokana na mahubiri yake aliyoyatoa kanisani hapo.

“Nilipoitwa, yale mashtaka ilikuwa mahubiri yangu kanisani, sikuwa na mashtaka yoyote zaidi ya niliyoongea kanisani. kusema kweli moja kwa moja sina kosa, nikaieleza kamati sioni kama imefanya vizuri sababu niliyoyasema niliongea madhabahuni,” amesema Askofu Gwajima.


Askofu Gwajima amesema kuwa, angekuwa na makosa kama kauli zake angezitoa nje ya madhabahu, lakini kwa kuwa aliyatoa madhabahuni hakutenda kosa, akidai hakuna mwenye mamlaka ya kuhoji yanayosemwa madhabahuni.

“Kama ingetokea nimezungumza nje ya madhabahu hii ni sawa sawa, lakini nilizungumza kanisani na hakuna mtu mwenye mamlaka ya kuuliza maswali juu ya imani ya mtu na ibada inayofanywa kanisani. Katiba inasema Serikali haijihusishi na kuendesha dini, haina dini lakini watu wake wana dini,” amesema Askofu Gwajima.


Askofu Josephat Gwajima akiwasili viwanja vya Bunge tayari kuhojiwa na Kamati ya Bunge
Akizungumzia tuhuma za kutoa taarifa za uongo kuhusu  chanjo ya UVIKO-19,  Askofu Gwajima amesema hakuruhusu waumini wake wachanje akidai hajapewa taraifa za kutosha juu ya athari za chanjo hiyo.

“Panapotokea suala kubwa Tanzania, Baraza la Maaskofu Katoliki huwa wanatoa waraka kuongoza watu wao, sisi baraza letu la maaskofu la ufufuo na uzima, tukaona sisi na waumini wetu hatutaingia kwenye suala la kuruhusu wachanje,” amesema Askofu Gwajima na kuongeza:

“Msimamo wetu moja kwa moja ni kwamba, hatujapewa taarifa ya kutosha kuhusu chanjo na madhara yake ya muda mfupi na mrefu. Kama kuna mtu anataka kutupa taarifa ajitokeze, lakini mpaka sasa hatujapata taarifa.”

Askofu Gwajima aliingia kwenye mgogoro na Serikali, Bunge na chama chake cha CCM, baada ya kuibuka hadharani kupitia madhabahu ya kanisa lake, kupinga chanjo hiyo, akidai kwamba hakuna utafiti rasmi uliofanyika kujua madhara yake.

Ambapo alidai baadhi ya watu wanaohamasisha chanjo hiyo, wamepewa fedha kutoka kwa baadhi ya mataifa ya nje ili kufanikisha mpango wa utoaji chanjo kwa watu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad