Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Bw. Donald Wright ameipongeza Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kutoa huduma bora za ubingwa wa juu baada ya kutembelea Idara ya Magonjwa ya Dharura na Idara ya Afya ya Magonjwa ya Akili.
Balozi Wright amesema ameshuhudia jinsi wataalamu wanavyotoa tiba kwa wagonjwa wa magonjwa ya dharura wanaofikishwa katika idara ya magonjwa ya dharura.
Katika ziara hiyo, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Muhimbili, Dkt. Hedwiga Swai alimweleza Balozi Wright kwamba hospitali imekuwa ikipokea wagonjwa kutoka mikoa mbalimbali nchini na kuwapatia matibabu ingawa ya kuwapo kwa upungu wa wataalamu wa afya.
“Pamoja na Hospitali kuwa na upungufu wa wataalamu wa afya, tumekuwa tukipambana kutoa huduma bora za ubingwa wa juu kwa wagonjwa wote wanaofika Muhimbili,” amesema Dkt. Swai.
Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura wa Muhimbili, Dkt. Juma Mfinanga alisema idara hiyo imekuwa ikipokea wagonjwa 200 hadi 300 kwa siku kutoka maeneo mbalimbali ya nchi pamoja na nje ya nchi.
Idara hiyo inatoa huduma za dharura pamoja na kufundisha wataalamu mbalimbali wanaotoa huduma za dharura nchini na nje ya nchi.
Mkuu wa Idara Dkt. Hendry Sawe wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) ambaye pia anatoa huduma za afya katika Kitengo cha Magonjwa ya Dharura Muhimbili amemweleza Balozi huyo, MNH inampango wa kuanzisha mafunzo ya ubingwa wa magonjwa ya dharura kwa watoto na kukuza utafiti wa tiba ya watoto dharura za afya.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Afya ya Akili, Dkt. Jessie Mbwambo alimweleza balozi huyo jinsi idara hiyo ilivyofanikiwa kutoa huduma kwa wagonjwa wa afya ya akili nchini.
Katika Idara ya Magonjwa ya Afya ya Akili, baadhi ya watu waliotibiwa kwa muda mrefu walitoa ushuhuda jinsi walivyopona na sasa wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.
Balozi Wright amefanya ziara katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS), Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambako ameelezwa jinsi tafiti za kudhibiti magonjwa mbalimbali zilivyofanyika. Utafiti huo umejumuisha magonjwa ya afya ya akili, malaria, kifua kikuu, ajali na magonjwa yasioambukiza.
Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Bw. Donald Wright akielekea katika Idara ya Magonjwa ya Dharura katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH). Balozi huyo amefanya ziara katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS), Hospitali ya Muhimbili, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ambako ametembelea miradi mbalimbali ya kudhibiti magonjwa yakiwamo ya afya ya akili, malaria, kifua kikuu na ajali.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Afya ya Akili, Dkt. Jessie Mbwambo (kulia) akifafanua jambo kwa Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Bw. Wright wakati alipotembelea Kitengo cha Tiba ya Uraibu na Heroini.
Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura wa Muhimbili, Dkt. Juma Mfinanga akieleza jinsi Kitengo cha kuhudumia watoto kinavyofanya kazi.
Mmoja wa maofisa wa Idara ya Afya ya Akili wa MNH akitoa maelezo kuhusu huduma za afya kwa balozi huyo.
Balozi Wright akitoka katika Kitengo cha Tiba ya Uraibu na Heroini katika Hospitali ya Muhimbili.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Afya ya Akili, Dkt. Jessie Mbwambo akizungumza katika mkutano uliohusisha taasisi tatu za MNH, MUHAS, Ocean Road na JKCI.