Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga wakiongozwa na Mbunge wa Jimbo la Lushoto Shaaban Shekilindi wamekataa kuivunja Mamlaka ya Mji Mdogo wa Lushoto, kwani kufanya hivyo ni kudumaza maendeleo ya wananchi wa mji huo, ikiwa ni pamoja na kuwanyima wananchi siku moja kuwa na Halmashauri ya Mji au Manispaa ya Lushoto.
Wakizungumza kwenye Baraza la Madiwani, walisema madiwani wenzao waliojadili jambo hilo na kufikia kuivunja mamlaka hiyo, hawakufanya hivyo kwa maslahi ya wananchi, bali matakwa yao binafsi, hivyo kwa niaba ya wananchi, wanasitisha jambo hilo kuanzia sasa.
"Haiingii akilini kuivunja Mamlaka ya Mji Mdogo wa Lushoto. Mamlaka ni mwanzo wa kuwa na Halmashauri na baadae Manispaa. Hivyo kuamua kuvunja Mamlaka ya Mji ni kukataa kusogeza maendeleo kwa wananchi na kuweza kuongeza utendaji kazi na kusogeza huduma kwa wananchi. Mimi napinga suala la kuvunja Mamlaka ya Mji Mdogo wa Lushoto" alisema Shekilindi.
Diwani wa Kata ya Lukozi Karim Mahanyu alisema siku Mamlaka ya Mji Mdogo Lushoto itakapokuwa Halmashauri ya Mji, itatoa nafasi Halmashauri ya Wilaya kuhamia upande mwingine, ambapo Jimbo la Mlalo linaweza kuwa ndiyo Halmashauri ya Wilaya, na Mji wa Lushoto ukawa Halmashauri ya Mji, hivyo mafungu ya fedha yatakayopelekwa kwa wananchi, yataongeza huduma kwa wananchi.
Diwani wa Kata ya Kwai Idd Kipande alisema kuivunja Mamlaka ya Mji Mdogo wa Lushoto ni kuwaondolea fursa wananchi wa wilaya hiyo sababu wataendelea kujibana kwenye eneo moja la halmashauri ya wilaya na kukosa kujitanua kwa kuwa na halmashauri ya mji ambayo italeta fursa nyingi kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Mathew Mbaruku aliungana na madiwani kukataa kuivunja mamlaka hiyo ambayo ilianza mwaka 2004 na kuanza kuhudumia wananchi 2008, huku yeye kwa nyakati tofauti akiwa Mwenyekiti wa Mamlaka hiyo na kusema kuivunja ni kuwasaliti wananchi.
"Kwa kuwa suala hili baada ya kupelekwa ngazi za juu lilikataliwa, na kututaka sisi tulipeleke kwa wananchi ili waseme kama wanaitaka Mamlaka ya Mji Mdogo Lushoto ama la! na kwa vile sisi humu ndiyo wawakilishi wa wananchi, basi tuna uwezo wa kuwasemea wananchi. Hivyo tunasema Mamlaka lazima iendelee na kuboreshwa ili iweze kutenda kazi zilizokusudiwa" alisema Mbaruku.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Ikupa Mwasyoge alisema Mamlaka ya Mji Mdogo Lushoto ilifutwa na madiwani kwa vile ilidumaa, kwani pamoja na mambo mengine ilishindwa kujiendesha kwa kukosa mapato.
Akizungumza na wandishi wa habari hizi mara baada ya kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mbaruku alisema ni kweli, Mamlaka ya Mji Mdogo Lushoto yeye alikuwa Mwenyekiti wake, na baadae uongozi uliofuata haukuwa madhubuti, na ikaanza kuyumba, lakini hiyo sio sababu, kikubwa ni kuiwezesha iweze kusimama na kusonga mbele.
"Mamlaka ya Mji Lushoto ilianzishwa mwaka 2004, na kufika 2008 ikaanza kazi rasmi. Pamoja na misukosuko, lakini ilikuwa inaendelea. Madiwani wa mwaka 2010 hadi 2015 walianza mchakato wa kuifuta Mamlaka hiyo, lakini madiwani wa mwaka 2015 hadi 2020 ndiyo walibariki kuifuta Mamlaka hiyo.
"Suala hilo lilipofika kwa Mkuu wa Mkoa wakati huo (Martin Shigela) alikataa kubariki kufuta mamlaka hiyo kwa kusema madiwani hawana mamlaka ya kuifuta, na kuagiza mchakato wa kuifuta ukaanze chini kwa kuwauliza wananchi. Lakini kwa vile sisi tupo kwa ajili ya wananchi, tumeamua Mamlaka hiyo iendelee kuwepo, na iwezeshwe kujiendesha kwa kupata mapato" alisema Mbaruku.
Kwa upande wake Katibu wa CCM Wilaya ya Lushoto Ramadhan Mahanyu ambaye alikuwepo kwenye kikao hicho, alisema hoja ya kutaka Mamlaka ya Mji Mdogo Lushoto iendelee kuwepo ilianza kwenye chama kupitia Kamati ya Madiwani wa CCM.
"Suala la kuendelea kuwepo Mamlaka ya Mji Mdogo Lushoto ni msimamo wa chama, na lilianza kwenye chama katika Kamati ya Madiwani ya CCM, na mimi niliunga mkono kuendelea kuwepo kwa mamlaka hiyo. Tunachotakiwa ni kuiboresha mamlaka hiyo kwa kuiongezea maeneo ya utawala, na kuona inajiendesha kwa kupata mapato.
Hata hivyo alisisitiza kwamba hoja kubwa ni mbili. Mosi, Mamlaka ya Mji Mdogo wa Lushoto ikue na kuwa halmashauri ili kuongeza nafasi kwa Serikali kuweza kuwahudumia wananchi. Pili, Mji wa Lushoto unakuwa kwa kasi. Na ili uweze kuongezeka vizuri ni vizuri ukawa halmashauri. Lushoto tumechelewa sana, sababu wenzetu Wilaya ya Korogwe walipata Halmashauri ya Mji, na Wilaya ya Handeni, nao walipata Halmashauri ya Mji" alisema Mahanyu.