CHADEMA yatoa msimamo mgombea urais mwanamke



CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeeleza msimamo wake kuhusu kuweka mgombea mwanamke katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Kikisema hiyo siyo ajenda muhimu kwa wananchi na kutaka ziangaliwe sifa za mgombea bila kujali jinsia yake.

Akizungumza na gazeti hili katika makao makuu ya chama hicho, Dar es Salaam juzi, Naibu Katibu Mkuu, Benson Kigaila, alisema kwa sasa chama hicho kinaendelea kujiimarisha katika maeneo mbalimbali kupitia mkakati waliouita CHADEMA Digital, na kwamba itakapofika muda wa kusimamisha wagombea wataangalia sifa.

“Hiyo siyo ajenda muhimu mbona ADC mwaka 2020 walisimamisha mwanamke, kwani nani alisema kwamba kuna ajenda na kuna vyama vingi vimeshasimamisha wagombea wanawake mara nyingi tu… mbona hatujasema, Anna Mgwhira aligombea kupitia ACT-Wazalendo si alikuwa mwanamke?” Alihoji Kigaila.

“Tutasimamisha mtu kwa uwezo wake na siyo kwa jinsia yake, na huyo mwanamke hatakiwi kuungwa mkono, kwa sababu ya jinsia yake anatakiwa kuungwa mkono kwa uwezo wake,” alifafanua.

Akizungumzia kuhusu suala la rufani ya waliokuwa viongozi katika Baraza la Wanawake (BAWACHA) katika chama hicho Halima Mdee na wenzake, Kigaila alisema bado chombo cha kufikia uamuzi wa suala hilo ambalo ni baraza kuu la chama hicho halijakaa kufanya uamuzi wa rufani yao.

“Baraza Kuu halijakaa kusikiliza rufani yao, litakaa na haitakuwa siri itatangazwa,” alisema.

Halima Mdee na wenzake 18 walitimuliwa uanachama na uongozi wa chama hicho mwaka jana, baada ya kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum kwa kile kilichodaiwa ni kukiuka msimamo wa chama hicho.


Hata hivyo walikata rufani kwa kile walichodai kuwa mchakato wa kuwavua uanachama haukuwa halali, ingawa mpaka sasa rufani bado haijasikilizwa huku wakiendelea na nafasi zao za ubunge.

Kuhusu hali ya kisiasa na uongozi ya chama hicho kutokana na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, kushtakiwa Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi na hivyo kukosekana katika uongozi wa chama hicho Kigaila alisema pamoja na kuendelea kupambana na kesi mahakamani lakini hakuna kilichoharibika kwa kuwa wapo viongozi wengine.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad